Jambazi anauguza majeraha mabaya baada ya jaribio lake la kupora nyumba moja katika kijiji cha Tuuti, Kaunti ya Bungoma kugeuka na kumletea balaa.
Kulingana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), mwanamume huyo aliyekosa kutambulika alipenyeza nyumbani kwa Zipporah Masika, aliyekuwa akijiandaa kuoga majira ya asubuhi.
Zipporah alikuwa akienda bafuni akiwa amebeba maji moto ndipo akakutana na mwizi huyo, aliyekuwa ameiba simu yake na mali nyingine baada ya kuchokora nyumba.
Ndipo mwizi huyo alipomsukuma, Zipporah alimchoma na maji ya moto usoni na kutoroka akiwa anapiga kamsa na kuwashutua majirani waliofika katika boma hilo.
Hata ingawa mwizi huyo alikuwa na majeraha usoni ya kuchomwa, wanakijiji walianza kumpiga kitutu na hata ingawa aliwalilia wamuonee huruma, hakusikizwa na kuzidi kuongezwa majeraha.
Wakati polisi walipofika pale, mwizi huyo alikuwa anatirikwa na damu kwa kukatwa kichwani na wanakijiji ambao walionekana kutaka kummaliza. Maafisa hao walimkimbiza mwizi huyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma, ambako kwa sasa yuko hali mahututi akijaribu kupigania uhai wake.
Chanzo - Tuko news
Social Plugin