Usafiri wa ndege, ni usafiri unaopendwa zaidi duniani licha ya kuwa wa gharama. Ni usafiri unaotumia muda mfupi kwa safari ndefu na ni salama kwa kiwango chake ukilinganisha na usafiri kama wa barabara.
Watengenezaji wa ndege wengi wamekuwa wakijaribu kubuni ndege bora za kisasa hasa za abiria, lakini suala la kasi ya ndege linazingatiwa kwa kiwango chake.
Wakati ndege ya kwanza ya abiria ikianza safari rasmi za kusafirisha abiria Januari 1, 1914, ikitoka St. Petersburg, FL na kutua Tampa, FL, mwendo wa kama kilometa 27, hakuna mtu aliyefikiria miaka 100 baadaye kutakuwa na ndege kubwa zinazobeba abiria wengi na zenye kasi kubwa.
Miongoni mwa ndege hizo zenye kasi zaidi duniani ni hizi 5
5. Airbus A380
Airbus A380 ni ndege kubwa zaidi ya abiria duniani zinazotengenezwa Ulaya na kampuni ya Airbus, ikiwa na upana mkubwa na injini kubwa nne.
Kabla ya kutangazwa kuanza mradi wa kuzitengeneza mwaka 1990 kufuatia utafiti wa miaka miwili, Boeng 747 zilikuwa zimekamata soko la abiria na kasi.
Lakini sasa kwa mujibu wa Graham Simons, mwandishi wa kitabu cha The Airbus A380: A History Hardcover anasema kila baada ya dakika saba, ndege ya A380 imepaa ama kutua mahali fulani duniani.
Kinachoisaidia ni kasi yake, ikitajwa kutembea kwa kasi ya ya kilometa 1184 kwa saa.
4. Boeing 777
Boeing 777 ni miongoni mwa ndege kubwa ikiwa na injini pacha zilizotengenezwa na Boeing Commercial Airplanes. Ikitumia injini za General Electric GE90 turbofan, Boeing 777 inaweza kukimbia kwa kasi ya kilomita 1200 kwa saa.
3. Boeing 787 Dreamliner
Ndege hii yenye uwezo wa kubea abiria mpaka 330 kwa mtindo wa viti vya watu wawiliwawili ni moja ya ndege zenye kasi duniani. Ina uwezo wa kutembea kasi ya umbali wa kilometa 1,249 kwa saa.
Ukiacha kasi yake hiyo, Boeing 787 Dreamliner inafahamika kama moja ya ndege zilizofanikiwa sana sokoni licha ya kutokuwa ya muda mrefu sana sokoni.
2.Aerospatiale Concorde
Ni ndege yenye muuundo mwembamba ukilinganisha na Dreamliner ama Airbus ikibeba abiria kati ya 98 mpaka 128. Aerospatiale Concorde ya kwanza kabisa kuruka, ilikuwa Machi 2, 1969. Ni ya muda kidogo lakini zimedumu kwa wakati wake kwenye soko.
Muundo wake na injini zake zinaiwezesha kupaa umbali wa mpaka kilometa 18 kwenda juu na inaweza kutembea kwa urefu huo lakini kwa kasi ya mpaka kilomita 2.180 kwa saa.
Zinaendelea kutajwa kwa kasi yake zikianza huduma ya kusafirisha abiria kibiashara Januari , kupitia Air France na British Airways kama wateja wake wakuu.
1. Tupolev Tu-144
Hizi ni ndege zenye kasi zaidi kuwahi kutokea duniani na ndege ya kwanza ya Supersonic. Tupolev Tu-144 ilikuwa ndege ya wasovieti wakati huo ikitengenezwa na Tupoleve na kufanya shughuli zake kati ya mwaka1968 mpaka 1999.
Ina urefu wa mita 65.7 sawa na futi 215 na inch 7 , urefu kwenda juu ni mita 12.55 sawa na futi 41 na inch 2. Ukiangalia ilikuwa ndefu kwa futi 12 zaidi na upana wa futi 10 zaidi ukilinganisha na Concorde.
Haikudumu sana sokoni kwa sababu ya rekodi zake za ajali, gharama kubwa za matengenezo, na kuhitajika kwake kwa uchache sokoni, kukaifanya kutumika zaidi kwenye majeshi. Ndege hii ina kasi ya kilomita 2575km kwa saa.
CHANZO - BBC SWAHILI
Social Plugin