Polisi katika eneo la Rangwe, Kaunti ya Homa Bay nchini Kenya wanamsaka mhubiri anayetuhumiwa kumuua mtoto mwenye umri wa miaka 10, baada ya kumnajisi kisha akamnyonga na kutupa mwili wake katika shamba la mahindi.
Mwanaume huyo anaripotiwa kumnajisi msichana huyo katika kijiji cha Kamuombo katika lokesheni ndogo ya Kamenya, Rangwe, siku ya Alhamisi, 3,2022 jioni.
Jamaa za Vivian Akoth wanasema alikutana na mshukiwa wakati alipokuwa ametumwa nyumbani kwa bibi yake kuchukua kibuyu cha kuteka maji.
Nyanya yake alimtambulisha mwanaume huyo kwa jina moja tu Abraham ambaye alisema alikuwa mgeni wake kutoka Kisumu.
Mwanaume huyo aliyekuwa amevalia kanzu ambayo mara nyingi huvaliwa na waumini wa Legion Maria alikuwa katika nyumba hiyo kwa maombi.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, mwanamume huyo anaripotiwa kumfuata msichana huyo nje, akamshambulia na kumnyonga katika shamba la mahindi na kumwacha na maumivu makali.
Mpita njia alitokea na kupiga kamsa ambapo msichana huyo alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Homa Bay, lakini alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu.
Chifu Msaidizi wa eneo hilo Lilian Ombai alisema kasisi huyo alikuwa kwenye misheni ya kuombea familia.
Afisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kaunti hiyo ndogo Monica Berege alisema wamemkamata mwanamke mzee ambaye anasemekana alikuwa na mshukiwa wakati tukio hilo lilitokea.
“Anaweza tu kumtambua mshukiwa kwa jina moja. Lakini alikuwa akifanya nini na mwanaume huyo nyumbani kwake ikiwa hamjui? Tunafanya kila tuwezalo kumkamata mshukiwa mkuu,” Berege alisema.
Chanzo - Tuko News