Mahakama kuu nchini Nigeria imemhukumu mkuu wa polisi nchini humo kifungo cha miezi mitatu jela kwa kutotii amri ya mahakama.
Uamuzi huo ulifuatia kesi ya afisa wa polisi ambaye alifutwa kazi mwaka 1992. Afisa huyo alipinga kustaafu kwake kwa kulazimishwa, na kuachishwa kwake kazi baadaye kulikataliwa kortini.
Mahakama iligundua kuwa Inspekta Jenerali Usman Alkali Baba anafaa kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela, isipokuwa atamrejesha kazini afisa huyo wa polisi.
Mpaka sasa jeshi la polisi limeshindwa kutekeleza agizo hilo.
Katika taarifa, msemaji wa polisi Olumuyiwa Adejobi alielezea uamuzi huo kuwa “wa kushangaza”. Alisema jeshi la polisi linasoma hukumu hiyo ili kujua hatua za kuchukua.
“Inafundisha kutambua kwamba kesi hiyo inamhusu afisa ambaye alifukuzwa kazi tangu 1992, miaka michache baada ya IGP wa sasa kujiunga na Jeshi la Polisi la Nigeria,” alisema.
Aliongeza kuwa “hukumu ya hivi majuzi zaidi juu ya suala hilo ilitolewa mnamo 2011 ambayo haipaswi kuwa chini ya usimamizi wa sasa wa jeshi”.
Social Plugin