Mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo kwa viziwi Tanzania, Kelvin Nyema, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya lugha za alama kwa wanafunzi na wakufunzi wa chuo cha afya Sumbawanga mkoani Rukwa chini ya ufadhili wa taasisi ya Nos Vies en Partage (NVep) inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation,Mark Bristow.
Mkuu wa Chuo cha afya na Sayansi Shirikishi, Dk. Emmanuel Mwilonga akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya chuo hicho kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa , Christina Mzena
Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa, Christina Mzena akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya lugha za alama kwa wanafunzi na wakufunzi wa chuo cha afya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Washiriki wa mafunzo hayo katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Bi.Christina Mzena
Taasisi ya Maendeleo kwa Viziwi Tanzania (TAMAVITA) imeendesha mafunzo ya siku tatu ya wanafunzi na wakufunzi wa chuo cha Maafisa tabibu kilichopo mjini Sumbawanga mkoani kuhusu matumizi ya alama za vidole kwa viziwi.
Mafunzo haya yamefanyika kutokana na sehemu ya fedha zilizotolewa na taasisi ya Nos Vies en Partage (NVep) inayofadhiliwa na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Barrick Gold Corporation,Mark Bristow, akiwa nchini hivi karibuni alikabidhi msaada wa dola 10,000 kwa taasisi ya TAMAVITA kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu wa Shirikisho la vyama vya watu wenye Ulemavu mkoani Rukwa (Shivyawata), Elina John, alisema kuwa mwitikio wa watu wenye ulemavu kujitokeza na kupata huduma za afya katika hospitali, vituo vya afya na zahanati umetajwa duni kutokana na wataalamu wengi wa afya kutokuwa na elimu ya alama za vidole hivyo kushindwa kuwahudumia kikamilifu na kutibu maradhi yanayowasumbua.
Alisema kutokana na uelewa duni wa mawasiliano kwa njia ya alama za vidole kati ya wataalamu wa afya na viziwi wanaokwenda kupata huduma kwenye hospitali na vituo vingine vinavyotoa huduma ya afya umesababisha viziwi kukosa matibabu au kutibiwa maradhi wasiougua.
"Hapa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa kuna mwenzetu mmoja alipewa madawa ya ugonjwa asiougua......sasa haya mafunzo yatasaidia sana kujenga uelewa kwa wataalamu hawa lakini pia viziwi watapewa tiba sahihi", alisisitiza Elina John.
Awali, Mtendaji mkuu wa TAMAVITA, Kelvin Nyema alisema kukosekana kwa ujuzi wa mawasiliano miongoni mwa wagonjwa (Viziwi) na wataalamu wa afya hivyo kukosa huduma stahiki pindi wanapofika hospitalini hivyo ndio maana waliona kuna umuhimu wa kutoa mafunzo wanafunzi wa mwaka wa tatu ili baada ya kuhitimu waweze kusaidia kutatua changamoto hiyo.
Naye, Katibu Tawala wa wilaya ya Sumbawanga, Christina Mzena aliyefungua mafunzo hayo aliwasihi wataalamu hao wa afya kufanya kazi kwa kuzingatia weledi wa kazi yao na kupunguza malalamiko yasiyo na tija kutoka kwa wagonjwa.
Social Plugin