Awali John Siagi Magesa akiomba kura.
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Novemba 18,2022 wamechagua John Siagi Magesa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ambapo amepata kura 332 akifuatiwa na mpinzani wake wa karibu Salim Abdalah Simba aliyekuwa anatetea kiti hicho ambaye amepata kura 160 na Halima Ismail Juma akipata kura 13.
Akitangaza matokeo hayo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Festo Kiswaga ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kahama amesema kuwa wapiga kura waliopiga kura walikuwa 510 kura zilizoharibika kura 5 na kura halali 505.
Kiswaga amewashukuru wajumbe kwa ushirikiano na demokrasia walioyoionesha katika uchaguzi huo ambao umefanyika katika ukumbi wa NSSF kwa uhuru na haki.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika nafasi hiyo John Siagi Magesa amewasihi wajumbe kuwa wamoja na kudumisha ushirikiano hali itakayosaidia kuendelea kukijenga chama hicho na kuahidi kufanya ziara za kutembelea kata kwa kata na matawi ili kubaini changamoto zinazoikabili jumuiya ya wazazi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha maendeleo ya chama hicho.
“Nimpongeze aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Salim Abdallah Simba kwa uongozi wake wa miaka mitano iliyopita nitashirikiana naye katika uongozi wangu sambamba na kuendeleza yale aliyoanzisha,”amesema Magesa.
Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Shinyanga Salim Abdallah Simba amempongeza Magesa kwa ushindi alioupata na kuwaomba wajumbe kumuunga mkono mwenyekiti aliyechaguliwa katika utekelezaji wa majukumu yake mapya ya kuiongoza jumuia hiyo kwa kipindi cha miaka 5.
Nao baadhi ya wajumbe walioshiriki uchaguzi huo kwa masharti ya kutotaka kutaja majina yao wameeleza kuwa wana imani kubwa na mwenyekiti aliyechaguliwa kuwa atawaletea maendeleo katika kipindi cha uongozi wake.
Msimamizi wa Uchaguzi, Festo Kiswaga akizungumza wakati wa mkutano wa uchaguzi
John Siagi Magesa akiomba kura
John Siagi Magesa akiomba kura
Salim Abdalah Simba akiomba kura
John Siagi Magesa na Salim Abdalah Simba
Halima Ismael Juma akiomba kura
Social Plugin