Mkuu wa Chuo cha waandishi wa habari na Utangazaji Fanikiwa Bw Andrea Ngobole akitoa hotuba kwa wahitimu.
NA ONESMO ELIA MBISE-ARUSHA.
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kujiajiri wao wenyewe katika sekta ya habari na utangazaji kwa kuanzisha vyombo mbalimbali vya mtandaoni kwa kuzingatia ukuaji wa teknolojia ili kuharakisha zoezi la kuipasha jamii habari kwa wepesi na haraka zaidi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Media Aid for Indigenous Pastoralist Community (MAIPAC) na mjumbe wa bodi ya MISA-Tanzania Bw. Mussa Juma akizungumza katika mahafali ya 16 ya Chuo cha Uandishi wa Habari na Uangazaji Fanikiwa yaliyofanyika katika ukumbi wa PPS jijini Arusha.
Bw. Musa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo amesema kuwa ulimwengu wa sasa umekua, hasa katika eneo la sayansi na teknolojia hivyo wana habari wanapaswa kukimbia na ukuaji huo kwa kuanzisha vyombo vya habari vya mitandaoni ambavyo vitawasaidia wao kujiajiri kitaaluma.
Hata hvyo ameeleza kuwa waandishi wengi wanaweza kufungua "Blog, radio mtandao na Tv za Mitandaoni ambazo wanaweza kupeleka maudhui mbali mbali ya kihabari na kupitia vyombo hvyo watapatikana wawekezaji mbalimbali ambao wataweka matangazo ya biashara zao ili zionekane na watazamaji au pengine wasomaji.
Mbali na hayo amewataka wahitimu hao wa ngazi ya Stashahada kuzingatia maadili wawapo kazini lakini pia kuwa wabunifu katika kuandika habari za mazingira,kilimo,uchumi, na hata mabadiliko ya hali ya hewa ili kusaidia kuwaweka katika mazingira mazuri zaidi ya kihabari.
Naye mkuu wa chuo hicho Bwana Andrea Ngobole, amewataka wazazi wa wahitimu hao kuwaendeleza zaidi vijana hao katika chuo kikuu ili waendelee kupata elimu zaidi juu ya tasnia ya habari na sekta nyinginezo.
Aidha katika Mahafali Hayo wahitimu wapatao 40 wamehitimu mafunzo yao ya umahiri katika Tasnia ya habari na utangazaji ambapo pia wamedhamiria kwenda kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya habari na utangazaji.