Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima (kushoto) akizindua Mwongozo wa Taifa wa uendeshaji majadiliano kuhusu Mila na Desturi zenye Madhara kwa Jamii.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kusaidia kupambana na matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambayo yameendelea kuripotiwa nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alitoa rai hiyo Jumanne Novemba 08, 2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha Maafisa Maedeleo ya Jamii wa Sektretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Maendeleo ya Jamii kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara.
Dkt. Gwajima alisema wataalamu hao wa maendeleo ya jamii wanao mchango mkubwa katika ustawi wa jamii hivyo baada ya kikao hicho wakaweke mikakati itakayosaidia kuwalinda wanawake na watoto ambao ni wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Katika kikao hicho, Mratibu wa mpango wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA), Joel Mangi alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimezidi kuongezeka nchini ambapo matukio 20,306 yakiwemo elfu nane ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu.
Mangi alibainisha kuwa matukio ya ukatili yalioongoza katika kipindi hicho ni mimba kwa wanafunzi yaliyofikia 1,115 pamoja na udhalilishaji wa kijinsia ambapo ubakaji ni matukio 4,797 na ulawiti matukio 1,044.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji shirika la kutetea haki za wanawake na watoto KIVULINI la jijini Mwanza, Yassin Ally alisema utendaji kazi wa maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya wilaya, mkoa na halmashauri ukiimarishwa watasaidia kuelimisha jamii kupitia vikao mbalimbali na hivyo kusaidia kutokomeza matukio ya ukatili.
Alisema ni vyema ukawepo mkakati wa kuwawezesha maafisa maendeleo ya jamii na kuhakikisha wanawafikia wananchi angalau mara mbili kwa kila wiki badala ya kukaa maofisini muda wote huku wakiacha kulalamika kwamba wamenyang’anywa majukumu yao na kada nyingine.
Yassin pia alishauri kuimarishwa kwa mikakati ya ulinzi wa watoto wa jinsia zote kufuatia idadi ya watoto wa kiume wanaolawitiwa kuongozeka, akisema changamoto hiyo imetokana na nguvu kuelekezwa zaidi kwa watoto wa kike.
Awali Rais wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Angela Mvaa alisema tayari mchakato wa kuanzisha Sheria ya Maendeleo ya Jamii umeanza ambapo kukamilika kwake kutasaidia wataalamu hao kutimiza kwa weledi majukumu yao.
Takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia zilizotolewa kwenye kikao hicho katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, zinaonyesha kuwa Mkoa wa Mbeya unaongoza kwa matukio 301 ya ubakaji, Morogoro na Mwanza kila mmoja matukio 114 ya mimba kwa wanafunzi na Mkoa wa kipolisi Kinondoni ukiongoza kwa matukio 96 ya ulawiti.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akifungua kikao kazi cha Maafisa Maedeleo ya Jamii wa Sektretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Maendeleo ya Jamii kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara kinachofanyika jijini Dodoma, Novemba 08-10, 2022.
Mratibu wa Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), Joel Mangi akitoa takwimu za ukatili kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2022.
Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wakifuatilia kikao kazi hicho.
Mkurugenzi Mtendaji Shirila la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto KIVULINI, Yassin Ally akitoa salamu kwenye kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yassin Ally wakati akiwasilisha mada kwenye kikao kazi hicho.
Washiriki wakifuatilia kikao hicho.
Maafisa Maedeleo ya Jamii wa Sektretarieti za Mikoa na Wakuu wa Idara za Maendeleo ya Jamii kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania Bara wakifuatilia kikao hicho.
Viongozi mbalimbali meza kuu akiwemo mgeni rasmi, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima (wa tatu kushoto).
Social Plugin