#Serikali kutoa ushirikiano kuendeleza Kituo cha AMGC
Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameutaka uongozi wa Kituo cha African Minerals and Geosciences Centre (AMGC) kianze kufikiria namna ya kuhusisha Madini ya Kimkakati yanayohitajika duniani kwa sasa kwa ajili ya ujenzi na uzalishaji.
Dkt. Biteko, amebainisha hayo leo Novemba 3, 2022 Jijini Dodoma alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha AMGC Ibrahim Shaddad kinachotoa huduma mbalimbali kwa wachimbaji wa madini, maabara na kutoa mafunzo kwa wachimbaji wa madini kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika.
Kikao hicho kilicholenga kujadili huduma mbalimbali zinazotolewa na kituo cha AMGC Dkt. Biteko amekitaka kiongeze ufanisi ili kukifanya kituo kiwe na thamani kubwa hapa Afrika.
Akizungumzia umuhimu wa Kituo hicho cha AMGC Dkt. Biteko ameutaka uongozi huo kuhakikisha unakua na ushindani Afrika na kuzishinda taasisi nyingine ambazo zinaweza kujitokeza.
"Mkurugenzi ametueleza maendeleo yaliyopo kwenye Kituo na changamoto wanazopitia ikiwemo baadhi ya wanachama wa kituo hicho kutochangia michango kwa wakati," ameeleza Dkt. Biteko.
Aidha, amemshauri Mkurugenzi Mkuu wa AMGC kuwapitia wanachama wa umoja huo kuchangia kwa wakati ili kituo kiendelee kutoa huduma zinazokusudiwa kwa wanachama wake.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa AMGC Ibrahim Shaddad ameahidi kutatua changamoto zilizopo kwenye Kituo hicho ili kuleta tija kwa wanachama wake. Aidha amesema AMGC itaongeza ufanisi katika utendaji kazi kama ilivyoelekezwa na Waziri wa Madini Dkt. Biteko katika kikao hicho.
Kituo cha AMGC kilianzishwa mwaka 1977 na kuwakilisha nchi mbalimbali hapa Afrika, Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali kwa wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa tija.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Adolf Ndunguru na Wataalam kutoka wizarani na taasisi zilizo chini ya wizara.
Social Plugin