Na Abel Paul- Jeshi la Polisi
Mkuu wa kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Arusha mrakibu wa Polisi SP Solomon Mwangamilo amewataka madereva wa vyombo vya moto kuwa makini katika matumizi ya vyombo hivyo pamoja na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali za mara kwa mara katika Mkoa wa Arusha.
Mwangamilo ametoa kauli hiyo leo Novemba 08 2022 wakati wa kukabidhi pikipiki kwa viongozi wa dini kutoka Manyara,Kilimanjaro pamoja na Arusha ambapo amesema kuwa viongozi wanaowajibu wa kutibu mioyo ya wanadamu kiroho na kuwaomba kutokubali kumvuta na shetani wakati wa matumizi ya vyombo hivyo.
SP Solomon ameongeza kuwa wao kama Jeshi la Polisi wana wajibu kutoa elimu kwa makundi yote ili kuwa na uelewa wa pamoja na kukomesha ajali mkoa wa wa Arusha.
Kwa upandee wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dk Barnabas Mtokambali amesema lengo la kutoa vyombo hivyo ni kuwafikia waamini wa dhehebu hilo na kutoa huduma ya kiroho na kazi za kanisa ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo ya kanisa hilo.
Wakati huo huo Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomon Mwangamilo amewataka madereva wa vyombo vya moto maarufu mando wanaofanya safari zao nje ya jiji la Arusha na kwenda maeneo ya vijijini kufanya marekebisho ya vyombo hivyo ili kupunguza ajali za mara kwa mara.
Akiwa katika kata ya Meserani wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha, Mwangamilo amezungumza na madereva wa vyombo hivyo ambapo amewataka kufanya marekebisho na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuondoa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo zinazosababishwa na vyombo hivyo maarufu Mando.