Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC MBONEKO AMUOKOA MWANAFUNZI KIDATO CHA PILI NDOA YA UTOTONI...AELEZA WALIVYOMDAKA MZAZI


 Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (kushoto) akiwa na mwanafunzi wa kidato cha pili ambaye amemuokoa asiozeshwe ndoa ya utotoni.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na mwanafunzi ambaye amemuokoa asiozeshwe ndoa ya utotoni.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amemuokoa mwanafunzi wa kidato cha pili (16) aliyekuwa akisoma katika shule ya Sekondari Solwa wilayani Shinyanga, ambaye alitoroshwa na wazazi wake kwa ajili ya kwenda kuozeshwa Mpanda mkoani Katavi.


Mboneko amebainisha hayo leo Novemba 9, 2022 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa, pamoja na kumtembelea mwanafunzi huyo katika Shule ya Sekondari Solwa, ambaye kwa sasa yupo mikononi mwa Serikali na anaishi na mwalimu shuleni hapo.

Amesema Oktoba 28 mwaka huu, alipokea taarifa kuwa kuna mwanafunzi wa kidato cha Pili katika shule ya Sekondari Solwa kwamba ametoroshwa na baba yake na kupelekwa Mpanda mkoani Katavi kwa ajili ya kuozeshwa, ndipo akafanya mawasiliano na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika- Katavi, na kufanikiwa kumkamata mzazi  na mtoto huyo huku muoaji akikimbia.

“Nilipopewa taarifa tu juu ya mtoto huyu kuwa ametoroshwa, siku hiyo hiyo nilifanya mawasiliano ya haraka na Mkuu wa wilaya ya Tanganyika tukawakamata na kufanikiwa kumrudisha mtoto huyu haraka shuleni na akafanya mtihani wake wa kidato cha Pili,”amesema Mboneko.

“Mwanafunzi huyu kwa sasa yupo chini ya Serikali na anaishi na mwalimu shuleni hapa, na hakuna hata kwenda likizo kwa wazazi wake, bali watakuwa wakija hapa shuleni kumsalimia na nitamsimamia hadi afike chuo kikuu na kutimiza ndoto zake,”ameongeza Mboneko.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya ameonya wazazi kuacha tabia ya kuozesha wanafunzi wa kike, bali wawaache wasome na kutimiza ndoto zao, na kubainisha kuwa wataendelea kufuatilia watoto wote ambao ni watoro shuleni, ili kubaini wanakabiliwa na matatizo gani pamoja na kuzuia ndoa za utotoni.

Naye Mwalimu ambaye anaishi na mtoto huyo kwa uangalizi zaidi Oliva Kalinga, amesema baada ya kumaliza mtihani wake wa kidato cha Pili wanaendelea kumpatia masomo ya ziada ili aendelee kuwa vizuri darasani.

Kwa upande wake mwanafunzi huyo ambaye (jina lake limehifadhiwa) amesema yeye anapenda kusoma, na ndoto zake ni kuja kuwa mwalimu, huku akimshukuru Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko kwa kuokoa ndoto zake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com