Muonekano wa Tope ambalo linatoka kwenye bwawa la Mgodi wa Mwadui ambalo limebomoka na kusambaa kwenye makazi ya watu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akizungumza na vyombo vya habari.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa habari
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akizungumza na waandishi wa habari
Muonekano wa Tope ambalo linatoka kwenye bwawa la Mgodi wa Mwadui ambalo limebomoka na kusambaa kwenye makazi ya watu.
Muonekano wa Tope ambalo linatoka kwenye bwawa la Mgodi wa Mwadui ambalo limebomoka na kusambaa kwenye makazi ya watu.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amesema katika tukio ambalo limetokea jana la bwawa la mgodi wa Almasi Mwadui kubomoka na kusambaza tope kwenye makazi ya watu, kuwa hakuna kifo ambacho kimetokea zaidi ya mashamba na baadhi ya Kaya kuathirika, huku Mgodi huo ukisimamisha kwa muda shughuli za uzalishaji Almasi.
Tukio hilo la bwawa la Mgodi wa Almasi Mwadui la kuhifadhia maji machafu kubomoka lilitokea jana Jumatatu Novemba 7,2022 majira ya saa 4 asubuhi, ambapo baadhi ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo vilipata madhara ikiwamo kuharibika mashamba na visima vya maji kufunikwa na tope.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 8,2022, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Dkt Sophia Mjema amesema watu walioathirika na tukio hilo ni 59, nyumba 13 zimezingirwa na tope, huku watoto watatu wakipata tatizo la kutapika na wameshapelekwa Hospitali kupatiwa matibabu.
Amesema vijiji ambavyo vimeathiriwa zaidi na tope hilo ni Ng’wangh’oholo, na Nyenze ambapo nyumba zao na mashamba zimeathiriwa zaidi na tope la mgodi huo, na tayari wameshapelekewa msaada wa chakula na maji, wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya tukio hilo.
“Mgodi wa Mwadui jana ulipata tatizo la bwawa lake kubomoka na kusambaza tope kwenye makazi ya watu, lakini tunashukuru hakuna kifo hata kimoja na mgodi umesimama kwa muda kufanya shughuli za uzalishaji Almasi hadi pale tutakapojiridhisha kuwa kuna usalama,”amesema Mjema.
“Nyumba ambazo zimezingirwa na tope ni 13, na wananchi walioathirika ni 59 na Kaya 19 na watoto watatu walipata shida kidogo ya kiafya na wanaendelea na matibabu, na Serikali tumeshaunda tume ambayo inachunguza tukio hilo na itakuja na majibu yote pamoja na kutoa tathmini ya ujumla,”amesema Mjema.
Aidha, akizungumzia juu ya madhara ya tope/udongo huo kwa binadamu, RC Mjema amesema uchunguzi tayari unafanyika ambapo sampuli zimeshachukuliwa, ili kuona kama kuna madhara yoyote ya binadamu.
Nao baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo akiwemo Tabu Kikuya mkazi wa kitongoji cha Manai kijiji cha Ng’wangh’olo, amesema walishangaa kuona tu tope zito likiwa limetapakaa na kuvamia makazi yao, huku mashamba na visima vya maji vikifunikwa, ndipo ikabidi wakimbie ili kuokoa maisha yao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Manai Ester Seni, amesema wanaiomba Serikali kufanya tathmini ya athari ambazo wamezipata wananchi, na waone namna ya kuwasaidia, pamoja na wataalamu kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini tope hilo kama linaweza kuleta madhara kwa wananchi kwa sababu limetoka ndani ya mgodi huenda kuna sumu.
Afisa Mahusiano Mgodi huo wa Almasi Mwadui Bernard Mihayo, amesema wao kwa sasa hawawezi kuzungumzia suala hilo, ambapo wamekubaliana msemaji wa tukio hilo atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema.