Meneja Mwandamizi Malipo ya Kadi na Kidigitali wa Benki ya CRDB, Victor Makere azungumza na wadau wa Sekta ya Utalii ikiwamo wadau kutoka Serikalini, wamiliki na wasimamizi wa kampuni za Utalii juu ya fursa zinazotolewa na Benki hiyo katika sekta ya utalii, wakati wa Maonyesho ya Utalii Barani Ulaya yaitwayo “My Tanzania Roadshows”.
======== ======== =========
Benki ya CRDB imedhamini na kushiriki maonyesho ya Utalii Barani Ulaya yaitwayo “My Tanzania Roadshows” yaliyofanyika kuanzia Novemba 12 -19 katika majiji manne barani ulaya; Amsterdam (Uholanzi), Paris (Ufaransa), Cologne (Ujerumani) na Brussels (Ubelgiji) yaliyoandaliwa na kampuni ya KILIFAIR ambayo ni kampuni ya kizawa inayojishughulisha na uandaaji wa maonyesho na warsha mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Maonyesho hayo ambayo yalikuwa na mvuto wa aina yake, yalitoa fursa kwa kampuni za utalii, mamlaka za utalii na wadau wengine nchini kufungua milango ya ubadilishanaji uzoefu, kujifunza tamaduni mpya, kuonyesha bidhaa za kitalii na kutangaza vivutio vinavyopatikana nchini.
Akizungumza katika moja ya Maonyesho hayo, Meneja Mwandamizi Malipo ya Kadi na Kidigitali wa Benki ya CRDB, Victor Makere alisema kupitia maonyesho hayo, Benki ya CRDB ilitumia fursa hiyo kuhudumia wateja wake wa diaspora (kampuni na watu binafsi) waliopo barani Ulaya vilevile kupitia jalada lake la wateja wa diaspora kutoa fursa ya kuhudumia wale wenye maono ya kutaka kuwekeza katika sekta ya utalii Tanzania.
"kupitia maonyesho haya tumeweza kukutana na wateja wetu katika sekta ya utalii ambao tumewawezesha na kuwajulisha juu ya njia za malipo zinazopatikana katika Benki ya CRDB ili kuwasadia wateja wao kufanya malipo kwa urahisi pale wafikapo nchini.”
Kupitia ushiriki wao katika maonyesho haya, Benki ya CRDB inaunga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii kwa kusogeza karibu huduma za kibenki zenye mlengo wa kusaidia kufungua njia na kuwarahisishia wawekezaji wa sekta hiyo.
--
Social Plugin