Viongozi wa dini nchini wamehimizwa kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti, mimba kwa wanafunzi na mauaji ambavyo vimeendelea kuripotiwa katika jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally wakati akizungumza kwenye kongamano la viongozi wa dini mkoani Mwanza lililofanyika Novemba 25, 2022 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Ally alisema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu na hovyo kuepuka kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kwamba wakitimiza wajibu huo ipasavyo watasaidia kutokomeza vitendo hivyo.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za jeshi la polisi nchini kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, kulikuwa na jumla ya matukio 8,396 ya vitendo vya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa ambapo matukio 6,986 yalihusisha wanawake huku matukio 1,410 yakihusisha wanaume.
Ally pia alitoa rai kwa wazazi na walezi kuwa makini katika malezi ya watoto wao hususani wa kiume ambao wamekuwa katika hatari kubwa ya kukumbwa na vitendo vya ulawiti akisema hapo awali nguvu kubwa ilielekezwa kwa watoto wa kike ambao walidhaniwa wako hatarini hivyo ni vyema uangalizi ukaelekezwa kwa watoto wa jinsia zote.
Naye Sheikh wa Mkoa Mwanza, Hassan Kabeke alisema ni vyema ikawepo mikakati ya pamoja itakayosaidia kuimarisha malezi bora na kuimarisha tabia njema katika jamii hatua itakayosaidia kuwa na kizazi salama.
Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli jijini Mwanza, Dkt. Jacob Mutashi alisema chanzo kikubwa cha vitendo vya ukatili wa kijinsia ni kukosekana kwa malezi bora katika jamii na hivyo kutoa rai kwa wazazi na walezi kutimiza wajibu huo huku akitoa rai kwa wanandoa kuepuka migogoro inayoweza kusababisha vitendo vya ukatili.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isaack Ndassa (kushoto) akizungumza wakati wa kongamano hilo ambapo alisema Serikali imekuwa ikiweka mikakati na jitihada mbalimbali ili kusaidia kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini, jeshi la polisi na taasisi binafsi wakifuatilia kongamano hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la KIVULINI, Yassin Ally akizungumza kwenye kongamano hilo.
Viongozi mbalimbali meza kuu wakiwa kwenye kongamano hilo.
Jumbe mbalimbali kutoka shirika la KIVULINI zenye lengo la kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Usijihusishe kimapenzi na wanafunzi maana kama unapenda sketi za shule mshonee mkeo/mmeo ili umpende kwa dhati na kuwaacha wanafunzi wasome.
Siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia huadhimishwa kimataifa kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10 kila mwaka kwa lengo la kuikumbusha jamii kujiepusha na vitendo hivyo hususani kwa watoto na wanawake ambao ni wahanga wakubwa.
Social Plugin