"Furaha yangu haitegemei" mwanamume, anasema Laura Mesi, ambaye anadai kuwa mwanamke wa kwanza wa Kiitaliano kujioa mwenyewe.
Hebu tafakari kula kiapo cha ndoa yako mwenyewe kwa kutumia maneno kama: 'Nimejisamehe' na 'sitajiita tena mbaya'.
Karibu katika ulimwengu wa ndoa ya kibinafsi au "mpenzi mmoja", ambao umepata umaarufu katika miaka michache iliyopita.
Ingawa ndoa ya kibinafsi haijahalalishwa mahali popote duniani, ripoti za watu kufanya sherehe za harusi binafsi imekuwa ikifanyika kwa miongo kadhaa.
Sologamy, sherehe ya harusi ambapo mtu huamua kujioa mwenyewe, imekuwa mtindo unaokua katika nchi za Magharibi katika miaka michache iliyopita.
Wanaounga mkono sherehe kama hizi wanasema ni ishara ya kujipenda na kujikubali, na kudai uthibitisho wa kijamii ambao kawaida huhifadhiwa kwa wanandoa waliooana.
Ingawa hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi ya wale wanaoamua kujioa wenyewe, hii ya watu kuzingatia mtindo huu wa maisha inakuja wakati ambapo idadi ya watu ambao hawajaoa au kuolewa inzaidi kuongezeka katika mataifa mengi ya kiuchumi mkubwa, kulingana wataalamu wa masuala ya kijamii.
1. Italia
Ili kupanga harusi ya peke yako, Bi Mesi anasema unahitaji pesa, usaidizi kutoka kwa wale walio karibu nawe - na zaidi ya yote "kichaa kidogo"
Mnamo mwaka 2017 mwanamke wa Kiitaliano kwa jina Laura Mesi alizua gumzo nchini humo alipoamua kujioa mwenyewe katika sherehe ya harusi iliyojumuisha viashiria vyote vya harusi ya wenzi wawili kama vile mavazi meupe, keki ya harusi ya gorofa tatu, bi harusi na wageni 70.
Laura anasema wazo la harusi ya peke yake lilimjia mwaka 2015, baada ya uhusiano wake wa kimapenzi wa miaka 12 kuvunjika
"Ninaamini kabisa kwamba kila mmoja wetu lazima kwanza ajipende," alisema Laura Mesi, mkufunzi wa mazoezi ya viungo mwenye umri wa miaka 40."
Japo sherehe hiyo haina uzito wa kisheria.
Bi Mesi alikuwa sehemu ya mtindo unaokua wa kujioa mwenyewe - unaoitwa "sologamy" - katika nchi tofauti duniani.
Bi Mesi anasema yeye ndiye mwanamke wa kwanza wa Kiitaliano kufanya sherehe ya harusi yake mwenyewe.
2. Japan
Nchini Japan, shirika la usafiri lilianza kutoa sherehe za harusi kwa wanawake wasio na waume mnamo 2014.
Shirika la habari la Kyodo liliripoti kifurushi maalum cha siku mbili cha "harusi yako mwenyewe" ya Cerca Travel iliyojumuisha kuchagua gauni lako maalum, shada la maua na staili ya nywele, huduma ya limousine, kukaa hotelini na albamu ya picha ya ukumbusho.
"Kifurushi hiki kiliongeza hali yangu ya kujistahi... athari ilikuwa sawa na uzoefu wa ajabu zaidi, kama vile kutembelea jumba la Urithi wa Dunia," anasema Tomoe Sawano, mmoja wa wateja wa kwanza kufanya "harusi yake mwenyewe".
Karibu nusu wanawake wanaoamua kujioa wenyewe walikuwa wanawake walioolewa ambao hawakufanyiwa sherehe ya harusi au hawakuridhika na uzoefu huo , kulingana na kampuni ya usafiri ya Cerca Travel.
Rais wa kampuni hiyo, Yukiko Inoue, aliiambia shirika la habari la Kyodo kwamba aliubuni kifurushi hicho "ili kuwahimiza wanawake kuwa na hisia chanya kuhusu wao wenyewe", lakini anakubali kwamba "baadhi ya watu wamesema itakuwa 'pweke, kuhuzunisha' kuitumia".
"Wajapan wengi wanaishi peke yao kwa sababu kadhaa - ikiwani pamoja na kuzeeka, ukuaji wa miji, umri wa kuolewa baadaye na viwango vya kuongezeka kwa talaka," Gazeti la The Japan Times lilisema katika makala iliyopita.
Lilinukuu Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Idadi ya Watu na Hifadhi ya Jamii likisema kwamba idadi ya watu nchini inatarajiwa kupungua kwa kati ya asilimia 26 na 38 ifikapo 2060.
3. Canada
Shirika linalofahamika kamaa Marry Yourself Vancouver ambalo limekuwa likiendesha ndoa za aina hii kwa miaka kadhaa sasa lnchini Canada linasema idadi ya watu wanaoamua kujioa wenyewe imekuwa kuongezeka.
4. Marekani
Nchini Marekani, tovuti inayoitwa I Married Me inatoa huduma ya kuwawezesha wanaoamua kujioa wenyewe kufanikisha azma hiyo.
Wanawake wa rangi na rika zote waliamua mtindo huuu wa maisha ya ndoa isiyo ya kawaida.
Mnamo 2015, Yasmin Eleby alijioa mwenywewe katika Jumba la Makumbusho la Utamaduni wa Kiafrika mjini la Houston siku mbili tu baada ya kuukaribisha mwaka mpya.
Alikuwa na umri wa miaka 40 alipoamua kuweka nadhiri ya kujifanyia harusi yake mwenyewe.
“Nilitaka kuwa na sherehe yangu mwenyewe. Harusi yangu mwenywe ambayo ingeangazia kujitolea kwangu binafsi kujipenda, kujiheshimu na kujua thamani yangu,” aliambia ABC News.
5. Uingereza
Nchini Uingereza, Sophie Tanner alijioa mwenyewe mwaka wa 2015. "Kwangu mimi, ilikuwa sherehe muhimu inayoonyesha kujitolea kwangu kujihurumia," aliambia BBC.
"Harusi ilikuwa siku muhimu zaidi maishani mwangu, iliyokamilika na gauni la zamani, baba aliyechoka kunipa, na wajakazi wanaocheza."
Lakini si kila mtu anakaribisha mwenendo wa sologamy. Wengine wanaiita kujipenda kupindukia na wengine wanaikosoa kama mtindo usio na maana kwa taasisi ya mfumo dume.
Karen Nimmo, mwanasaikolojia wa kimatibabu huko New Zealand, anasema: "Kutojipenda ndio chanzo cha maswala mengi ya kisaikolojia, kwa hivyo kujioa ni ni sehemu ya kupata uponyaji kutokana kwa kiwewe cha zamani au maswala ya uhusiano yaliyotibuka.
"Lakini ni muhimu kuhakikisha kuwa mahusiano yako mengine ni mazuri. Ikiwa unajitegemea sana na kuweka mahitaji yako mwenyewe mbele ya kila mtu mwingine unaweza kuwa unaingia katika hali mbaya- na hip ni mahali pabaya panapoweza kukaribisha upweke." Alexandra Gill, mwanzilishi mwenza wa shirika la ushauri Marry Yourself Vancouver, anaafiki kuwa kujioa kama "aina ya" ubinafsi uliopitiliza.
CHANZO - BBC SWAHILI