Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) inaandaa kozi mpya zitakazowezesha jamii kuendana na Mapinduzi ya nne ya viwanda ambazo zitasaidia kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Mkuu wa Taasisi Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam Prof. Ezekiel Amri katika ufunguzi wa warsha kwa wadau iliyofanyika kampasi Kuu ya Dar es salaam yenye lengo la kukusanya maoni kwa ajili ya kuboresha mitaala ya kufundishia kozi hizo katika ngazi ya Uzamili na Stashahada.
Prof. Amiri amezitaja kozi hizo kuwa ni Uzamili katika Uhandisi Komputa, Uzamili katika Uhandisi Mawasiliano Angani, Uzamili katika Usalama wa Kimtandao pamoja na Stashaha ya Mitambo Viwandani.
Prof Amir ameeleza kuwa, DIT imeaanda warsha hiyo ili kupata maoni ya Wadau kulingana na mahitaji ya soko la ajira ambapo amesema kuwa maoni yao yatatumika katika kuandaa mitalaa itakayoendana na mapinduzi ya nne ya viwanda pia kusaidia kutatua changamoto katika jamii.
“Mapinduzi ya nne ya viwanda yanaenda kasi sana na yamejikita katika Tehama, ni muhimu kujiandaa kwa kuwa na mitaala yetu inayoendana na mapinduzi haya ili tusibaki nyuma ". Amesema Prof Amir
Ameeleza kuwa, mapinduzi hayo yana fursa na changamoto za kufanyia kazi hivyo kwa kuboresha mitaala hiyo itawawezesha vijana watakaosoma kozi hizo kuendana na mapinduzi hayo kwa kuwa wataenda kukidhi mahitaji yaliyopo viwandani na kwenye jamii.
Prof Amir ameendelea kusisitiza kuwa, taasisi imeona umuhimu na mahitaji ya kozi hizo na namna ambavyo itawawezesha vijana katika soko la ajira na hiyo ndiyo sababu iliyopelekea kuandaa mitaala itakayoendana na mabadiliko hayo.
Aidha, amewataka wadau kutoa maoni yao kutokana na wanachokiona kwenye jamii kwa sasa na mbeleni kwa kuwa maoni yakiwa mazuri ndiyo yatakayozalisha mitaala bora. Amesema “Uwepo wenu katika warsha hii ni muhimu sana, maoni yenu ni ya muhimu kwani mawazo mtakayoyatoa yatasaidia uboreshaji wa mitaala hii”.
Naye Mratibu wa program hiyo ya kuandaa mitaala, Daktari Paul Mbaga amesema kuwa kikao hicho ni muhimu kwani nia kubwa ni kuiwezesha DIT kuja na mitaala itakayotatua changamoto zilizoko katika jamii.
“Ninyi mtatusaidia kuona tunachokiandaa kama kitafaa katika jamii katika kutatua changamoto za jamii na ndio sababu kubwa iliyopelekea kuwaomba mshiriki kwenye zoezi hilo.
Warsha hiyo iliyofanyika kwa siku moja imeshirikisha wadau kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.
Social Plugin