*************************
CHAMA Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimeunga mkono na kumpongeza Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson kwa hatua yake ya kuitaka Serikali kuangalia upya utaratibu utakaoruhusu mabasi ya abiria kusafiri usiku.
Akizungumza Dar es Salaam Mweka Hazina wa Taboa ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Usalama Barabarani Taifa Issa Nkya amesema wanaungana na Dkt Tulia katika hilo kwani ni jambo ambalo hata wao wamezungumzia kwa muda mrefu.
Awali akizungumza suala hilo hivi karibuni wakati aliposhiriki Semina kwa Wabunge kuhusu usalama Barabarani iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Jijini Dodoma, Dkt Tulia alisema haoni tatizo kutoruhusu magari ya abiria kutembea usiku ikiwa magari mengine tofauti na ya abiria yanafanya hivyo.
Dkt Tulia alisema ni wazi kuwa hatua hiyo ya kuyazuia magari hayo pamoja na mambo mengine kinarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi na kutaka wanaohusika kuangaliwa upya utaratibu huo ili kama kuna kikwazo chochote kiweze kutafutiwa ufumbuzi.
“Kuna shida gani ya kuzuia gari ya abiria kusafiri usiku? Tunatamani nchi yetu kuchangamka zaidi kiuchumi sasa kwanini magari haya yawe na zuio wakati magari mengine yanaruhusiwa kusafiri hadi usiku, Kama ni changamoto ya miundombinu basi ishughulikiwe na kama ni usalama Polisi wapo Cha msingi wekeni utaratibu huo ili shughuli zifanyike,” alisisitiza Dkt. Tulia
Aidha kauli ya Dkt Tulia imekuja ikiwa imepita miezi takribani tisa tangu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa azungumze Bungeni kuwa haoni tatizo lolote kwa mabasi hayo kusafiri usiku akisisitiza kuwa hatua hiyo itazidi kuchochea ukuaji wa uchumi.
Alitoa kauli hiyo Februari 10 ambapo alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) kujiridhisha na hali ya Usalama sambamba na kuzitaka Mamlaka zote zinazohusika kuweka utaratibu utakaofanikisha suala hilo.
Kwa upande wao TABOA kupitia kwa Mweka Hazina wake Nkya, alisema wao hawaoni tatizo la mabasi hayo ya abiria kutembea usiku na mchana na kwamba wao kama wasafirishaji ni jambo ambalo wamelipigania kwa muda mrefu.
"Kama alivyosema Spika wa Bunge Dkt Tulia, Kuna faida nyingi za kuwa na utaratibu wa kusafirisha abiria Kwa nyakati zote usiku na mchana, watu Kwa sasa wanafanya shughuli za kiuchumi usiku na mchana hivyo kuweka utaratibu wa kusafiri mchana peke yake ni kurudisha nyuma juhudi hizo" amesema Nkya
Amesisitiza wao kama wasafirishaji watakuwa wa watu wa kwanza kutoa ushirikiano utakaohitajika ili suala hilo liweze kufanikiwa ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wanachama wao wote nchi nzima ili huduma ambazo watatoa kwa massa yote 24 ziweze kuwa na ufanisi na siyo kuifanya kuwa changamoto.
Social Plugin