Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI UDOM WAASWA KUISHI KWA KUZINGATIA MAADILI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walioshiriki Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.


Baadhi ya Wanafunzi na Watumishi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao wakati akifunga Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.


Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mhandisi Joseph Mwaiswelo akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU) kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati wa Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga.


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kuzungumza na washiriki wa Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.


Mtendaji Mkuu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Patrick Ntwina, akitoa neno la utangulizi kabla ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi kufunga Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja na Jumuiya wa Wanafunzi Wapinga Rushwa ya Chuo Kikuu Dodoma mara baada ya kufungua Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga Jijini Dodoma.

**************************

Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe 27 Novemba, 2022

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuishi kwa kuzingatia maadili ya kitanzania ili kutimiza malengo yao kitaaluma na kujenga taswira nzuri ya chuo katika jamii.

Mhe. Ndejembi ametoa nasaha hizo jijini Dodoma, wakati akifunga Kongamano la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho lililofanyika katika ukumbi wa Chimwaga.

Mhe. Ndejembi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua kusimamia utawala bora, kuzingatia maadili na ndio maana inapinga vitendo vya rushwa hivyo, wanafunzi wa UDOM wanapaswa kuzingatia maadili mema kwa lengo la kujenga taswira nzuri ya chuo, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kujenga taifa lenye uadilifu.

“Mnapaswa kuishi kwa kuzingatia maadili ya Kiafrika na Kitanzania kwa sababu tabia zote mbaya mtakazozifanya, jamii haitowaelewa na itakishushia hadhi Chuo Kikuu cha Dodoma ambacho Serikali inakitegemea katika kuzalisha rasilimaliwatu yenye tija katika maendeleo ya taifa,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, hata chuo kikiendelea kuwa na matokeo mazuri ya wanafunzi kwa kiwango kikubwa lakini wanafunzi na watumishi wa chuo wasipoishi kwa kuzingatia maadili itakuwa ni sawa na kazi bure kwani hakitakuwa na hadhi mbele ya jamii.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo vya rushwa katika kipindi chote wanapokuwa chuoni na hata baada ya kuhitimu.

Mhe. Ndejembi amewataka washiriki wa kongamano hilo, kuhakikisha wanafanya mjadala utakaolenga kulinda na kukuza maadili kwa maslahi mapana na mustakabali wa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mhandisi Joseph Mwaiswelo amesema kuwa, vitendo vya rushwa vikipuuzwa vitaathiri taifa kimaadili na kukwamisha juhudi za maendeleo.

Naye, Mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Bw. Henry Magodi kwa niaba ya wenzie, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuwahimiza kuzingatia maadili na kupinga vitendo vya rushwa ili wawe ni sehemu ya watanzania wazalendo wenye nia thabiti ya kutoa mchango wa maendeleo katika taifa.

Kongamano hilo la Kukuza Maadili na Elimu ya Mapambano Dhidi ya Rushwa lililofungwa na Mhe. Deogratius Ndejembi, ni sehemu ya Maadhimishio ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo kilele chake ni tarehe 10 Disemba, 2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com