Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (aliyevaa miwani) akikagua na kupata maelekezo kutoka kwa Afisa wa WMA katika Chumba maalum cha vifaa vya uhakiki wa vipimo vya Mita za Umeme vilivyopo Misugusugu mkoani Pwani, anayeshuhudia katikati ni Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Pwani, Alban Kihulla. Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Pwani, Alban Kihulla akitoa maelekezo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira waliotembelea Kituo cha uhakiki wa vipimo, kilichopo Misugusugu mkoani Pwani. Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (kulia) akiteta jambo na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilipotembelea Taasisi hiyo katika Kituo cha uhakiki wa vipimo, Misugusugu mkoani Pwani.
*************************
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imewashauri Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kujenga vituo mbalimbali vya uhakiki wa vipimo vya dira za Maji, Umeme na Malori ya Mafuta kama inavyofanyika kwenye Kituo cha uhakiki wa vipimo hivyo, Misugusugu mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea Kituo hicho kilichopo Misugusugu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. David Kihenzile amewapongeza WMA kwa kazi nzuri inayofanyika ya kutoa huduma bora tangu kuanzishwa Kituo hicho mwaka 2019.
“Kamati tunawapongeza WMA kwa kazi nzuri inayofanyika hapa, lengo sio kumpa Mlaji kitu kisicho bora, lengo tuhakikishe Mlaji anapewa kile kilicho bora, Mfano kwenye uhakiki wa Mita za Maji na hata Mita Umeme, uhakiki uwe wa vipimo stahiki”, amesema Mhe. Kihenzile
Mhe. Kihenzile ameongeza, “Tunashauri vituo hivi viongezwe katika Kanda mbalimbali nchini ili kurahisisha utoaji huduma ya uhakiki na kumlinda Mlaji na yule anayetoa huduma”.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amesema kuwa mtoa huduma na Mlaji wananufaika na vipimo stahiki kupitia Taasisi hiyo ya Wakala ww Vipimo ambayo ipo chini ya Wizara hiyo.
Mhe. Kigahe amesema Serikali kupitia Wizara hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa Taasisi zake mbalimbali ili kuhakikisha Wananchi wananufaika na fedha za Kodi wanazolipa katika nchi yao.
“Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imetutembelea hapa kwenye Kituo cha uhakiki wa vipimo mbalimbali, tutajitahidi kuwaomba kuongeza Bajeti katika mwaka wa fedha ujao ili Taasisi zetu ndani ya Wizara yetu ziongezewe nguvu ili kufanya kazi kwa ufanisi wa hali juu”, amesema Mhe. Kigahe.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Wakala wa Vipimo (WMA) Bi. Stella Kahwa amesema watahakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa Watoa huduma na kuhakikisha Walaji wa mwisho wa huduma hizo wanalindwa.
Bi. Kahwa amesema ujio wa Kamati hiyo ya Bunge, ni fursa kwao WMA na endapo wataongezewa Bajeti katika Taasisi hiyo watahakikisha wanatumia vizuri katika kuboresha mazingira ya Ofisi zake sehemu mbalimbali nchini ili kufanya uhakiki wa vipimo sahihi, kuboresha vitendea kazi na Watumishi wake.
Kituo hicho cha uhakiki wa Vipimo vya dira za Maji, Umeme na Malori ya Mafuta kilijengwa mwaka 2019 katika eneo la Misugusugu, mkoani Pwani ambapo kimekuwa mfano mzuri na kuigwa kwa nchi jirani za Malawi, Uganda, Kenya Zambia katika utoaji mzuri wa huduma zake za uhakiki wa vipimo hivyo.
Social Plugin