Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomon Mwangamilo
***
Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha kupitia kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, limewaonya baadhi ya mawakala wanaopandisha nauli kiholela kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kuwa halitowafumbia macho wao pamoja na wamiliki wa magari hayo.
Akizungumza hii leo Desemba 13, 2022, katika kituo kikuu cha mabasi yaendeayo mikoani, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Arusha SP Solomon Mwangamilo, amesema kuwa kwa sasa tiketi zinakatwa kwa mfumo wa kielektroniki ambapo amebainisha kuwa hatopenda kusikia wamiliki na wakala wa mabasi hayo hawafuati utaratibu na maelekezo ya serikali.
Mwangamilo ameleza kuwa endapo atasikia mwananchi analalamika juu ya kupandishiwa nauli hatua kali zitachukuliwa kwa wakala atakayebainika kukiuka maagizo ya serikali pamoja na mliki kushindwa kusimamia watendaji wake.
Nae Yahaya Mbwana ambaye ni dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Singida na Arusha amewataka madereva wenzake kufuata sheria za usalama Barabarani ili kuepusha ajali ambazo chanzo chake ni ukikwaji wa sheria za usalama barabarani.
Nao baadhi ya mawakala wa mabasi yaendayo mikoani wamesema changamoto kubwa kutoka kwa abiria wao ni uelewa mdogo juu ya mfumo mpya na bei elekezi ya serikali ambapo wamesema imekuwa chanzo cha malalamiko kwa abiria.
Chanzo - EATV
Social Plugin