MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amewataka wanasiasa nchini kuacha kubeza na kupotosha jitihada zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kukopa huku wakijua fika kwamba ili Nchi ikopesheke ni lazima iwe imekidhi vigezo vya kiuchumi vya kupatiwa mikopo hiyo.
Ditopile ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema kitendo cha Tanzania kukopesheka kimeonesha jinsi gani Nchi yetu inaaminiwa.
" Nchi haikopesheki tu hovyo kuna mambo ya kiuchumi lazima yazingatiwe, jambo la kwanza inaangaliwa na kupitiwa taarifa ya ustahimilivu wa deni kwa miaka 10 iliyopita na baada ya kuridhika na ustahimilivu huo pili inaangaliwa matarajio ya miaka 20 ijayo. Mchakato huo unaangaza uwiano wa pato la mwaka na uuzaji wa bidhaa zetu nje pamoja na pato la mwaka na deni la Taifa ambapo ili ufuzu viwango vya kukopesheka Tanzania inapaswa uwiano huo usizidi asilimia 55.
Kwa takwimu za Benki ya Dunia na IMF, zinaonesha uwiano wetu Tanzania upo chini ya asilimia 30 ambayo ni hali nzuri sana na itachukua zaidi ya vizazi viwili kufikia hiyo asilimia 55 na zaidi ya vizazi vinne kufikia asilimia 75 ambacho ndio kiwango hatari cha ukopeshaji," amesema Ditopile.
Mbunge Dtopile ameongeza kuwa," " IMF na Benki ya Dunia zimeipongeza Nchi yetu kwamba pamoja na mlipuko wa Uviko-19 na vita ya Urusi na Ukraine uchumi wetu umekua mstahimilivu na haujatetereka hata kidogo. Na kwamba hali yetu ya deni na kukopesheka ipo vizuri. Niwasihi Watanzania wenzangu tuendelee kumuombea na kumuunga mkono Rais wetu.
Mbunge Ditopile amewataka watanzania kuwapuuza wanasiasa ambao wanafanya upotoshaji kuhusu mikopo ambayo Serikali inakopa na kwamba mikopo hiyo inakopwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa watanzania.
" Rais wetu Dkt. Samia hajikopei kwa mambo yake binafsi anakopa kwa lengo zuri la kuleta maendeleo kwa watanzania, na kukopesheka ni sifa nzuri kwa kuwa unaaminika na ni mlipaji mzuri.
"Wapo pia baadhi ya wanaobeza safari za Rais nje Nchi lakini niwaambie kupitia safari hizo uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje umeongezeka, uwekezaji wa ndani, uwekezaji wa pamoja kati ya wazawa na wageni umeongezeka mara nne ndani ya miezi mitano iliyopita. Miradi 132 yenye thamani ya Sh Trilioni 7, 50 (FDI), 30 uwekezaji wa ndani na 52 ya wazawa na wageni.
Chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Nchi yetu imerudishwa kwenye mpango wa fedha za MCC ambapo ziara yake nchini Marekani Novemba mwaka huu imezaa matunda na sasa tumerudishwa kwenye mpango huo ambao wote tunakumbuka miaka ya nyuma ulituwezesha kwenye miradi ya REA na Barabara ya Dodoma-Kondoa-Babati hadi Minjigu," amesema Ditopile.
Ameongeza kuwa ziara ya royal tour iliyofanywa na Rais Dkt Samia imezaa matunda mazuri kwani vivutio vyetu vya Utalii vimeweza kung'aa duniani ambapo Zanzibar na Arusha vimekua ndani ya vivutio 21 bora duniani.
" Februari mwaka huu Rais Dkt Samia wakati wa ziara ya falme za kiarabu kwenye maonesho ya biashara ya Dubai ameshuhudia utiaji wa saini ya hati ya makubaliano za miradi 36 ambayo Ina thamani ya Sh Trilioni 17.8.
Miradi hiyo imelenga kutoa ajira 204,575 hadi kufikia mwaka 2026, hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wetu katika kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kupitia diplomasia ya uchumi, kuvutia wawekezaji wa nje kuipa nguvu sekta ya utalii bila kusahau uuzaji na usafirishaji wa bidhaa zetu nje," amesema Ditopile.
Amewataka watanzania kuendelea kufanya kazi na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwani ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake ametekeleza mambo makubwa katika kila sekta ikiwemo Elimu, Afya na Maji.