Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Yusufu Makamba amempinga hadharani Katibu Mstaafu mwenzake Dk Bashiru Ali kuhusu kupinga kauli ya kuupiga mwingi huku akikemea matumizi mabaya ya neno 'Kuupiga mwingi' akisema maneno hayo yanapaswa kutumika kwa Marais tu ambao ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.
Akitoa salamu katika mkutano mkuu wa CCM jijini Dodoma leo 8, 2022 jijini Dodoma alipopewa nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM amesema :
"Wanaoupiga Mwingi katika nchi hii ni wawili tu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi.... nyinyi wengine ni Majembe tu, Eti unasema Mkuu wa Mkoa anaupiga mwingi, ana hela??".
"Hakuna mwingine wa kumpinga Rais Samia Mwaka 2025 ndani ya chama na hata kwa wanaotaka kuwania kiti hicho kutoka nje ya CCM kwani bado anaamini ana sifa za kuwa kiongozi",amesema.
Neno kuupiga mwingi, limekuwa likitumiwa na makada wa CCM wakimsifia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazofanya.
Novemba mwaka huu, Dk Bashiru akihutubia mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) uliofanyika mkoani Morogoro, aliwataka wakulima kudai haki zao, huku akionyesha kukerwa na kauli ya kuupiga mwingi.
Mkongwe huyo ambaye amejiita jina la Tobo, amemweleza Dk Bashiru kuwa aachane na kauli zake kwamba Rais Samia ni jembe badala yake akubaliane na waliowengi kuwa anaupiga mwingi.
“Jana nilimwambia Bashiru, wewe kipindi cha Magufuli (Hayati John) ulimuita buldoza sasa wenzako wakimuita kaupiga mwingi nongwa iko wapi,” amesema Makamba.