Mfano wa picha ya wanawake wanaojiuza
Afisa Mtendaji kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Suzana Kayange akizungumza na Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Ilikuwa ni jambo la kawaida kabisa kumkuta baba wa familia akiwa katika kijiwe cha kahawa au akicheza mchezo wa bao au drafti nyakati za asubuhi katika kata ya Mwamala halmashauri ya Shinyanga lakini sasa mambo ni tofauti!.
Licha ya mafanikio hayo lakini sasa changamoto iliyobaki ni kumaliza changamoto ya tabia ya wanawake waliopewa jina la ‘Nzige’ kufika katika kata hiyo kuuza miili yao kwa vijana na wazee hali inayoongeza umaskini na kuleta magonjwa ya zinaa ndani ya familia.
Malunde 1 blog imetembelea kata hiyo na kuzungumza na wakazi wa eneo hilo ambao wanasema kitendo cha wanaume kushinda kwenye vijiwe hakipo tena baada ya serikali kuingilia kati na kupiga marufuku tabia ya kushinda kwenye vijiwe muda wa kazi lakini changamoto iliyobaki ni Kudhibiti Nzige ‘wanawake wanaofika kijijini na kuuza miili yao’.
Wakazi wa kata ya Mwamala wanawaomba wanaume kutimiza majukumu yao ikiwemo kuwatunza wake zao ili kuachana na tama ya kuanzisha mahusiano na wanawake wengine
Mkazi wa Mwamala, Rebeca Edward anasema wanaume wasio na msimamo ndiyo wamekuwa wakirubunika na kuchukua mali za familia na kwenda kuzihonga kwa wanawake wanaouza miili yao kipindi cha mavuno hali inayosababisha baadhi yao kutelekeza familia zao.
“Japo hali ya uvamizi wa nzige imepungua kwa kweli inatuathiri sana sisi akina mama. Tunaomba serikali iendelee kuweka mkazo ili kuondoa kabisa vitendo hivi ambayo vinasababisha mali za familia kupotea lakini ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kupata maambuzi ya Virusi vya Ukimwi (VVU)”, amesema Rebeca.
“Wanaume tutunzeni , mtujali kama mlivyokuwa mnafanya kabla ya kutuoa, tunaomba mtujali badala ya kuhangaika na wanawake wengine wanaong’aa huko sentani. Msijisahau kwani tukitunzwa na sisi tutameremeta kama hao wengine, msitutelekeze, msitukimbie”,amesema Rebeca.
Magdalena Charles na Mwajuma John wanaongeza kuwa vitendo vya wanaume kuchukua mali za familia na kuzihonga hakikubaliki serikali inapaswa iweke sheria za kukomesha vitendo hivyo.
“Akina mama tunahangaika na watoto, bado kuna wanaume wanakimbia familia na kukimbilia sentani kufanya mapenzi na nzige. Ugomvi unatokea anapotaka kuuza mali za familia”,ameongeza Nyamizi Manoni.
“Hili suala la wanaume kuuza mali za familia na kuhonga machangudoa tulishaliongelea sana lakini hawasikii. Tumeshaongea tukachoka, tukiongea sana tunapigwa makofi, tunatelekezwa, serikali iangalie namna ya kumaliza tatizo hili”,amesema Kulwa Malale.
Ngasa Mhoja anawataka wanaume kuacha ubabe na tabia ya kuuza mali za familia na kwenda kufanya mapenzi na wanawake wanaojiuza kwani kitendo hicho ni sawa na kuibia familia.
“Wanaume wanaofanya hivyo wapo kwenye matumizi mabaya ya mali za familia kutafuta wanawake kwenye senta. Hawa wanawake wanaotafuta waume za watu nao wanatakiwa tu washughulikiwe kwani wanasababisha umaskini katika familia na kuleta magonjwa ndani ya familia”,amesema Bundala Pius .
Kwa upande wake, Mboje Malale (77) amesema wapo baadhi ya wanaume wanaoharibu familia zao kwa kuuza vyakula vya nyumbani. “Tunafanya siyo halali kuuza vyakula vya familia, ukiuza chakula cha familia unaharibu familia yako mwenyewe. Tusiendeleze haya mambo”.
“Familia zinatelekezwa kutokana na baba kupenda machangudoa wanaokuja senta wakati wa mavuno. Ni tamaa tu kwa wanaume”, amesema.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Wela kijiji cha Mwamala B kata ya Mwamala, Giti Singu Giti amesema ni kweli nyakati za mavuno huwa kuna wanawake ‘ Wasimbe’ maarufu Nzige huwa wanafika kwenye maeneo ya Senta na kuuza miili yao hali inayosababisha vijana na wazee kuuza vyakula nyumbani wapate pesa ya kulala na wanawake hao hali ambayo wamekuwa wakiikemea mara kwa mara kwani inaharibu familia.
Afisa Mtendaji kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Suzana Kayange amesema wamezuia wanaume kushinda kwenye vijiwe na migahawani muda wa kazi na wanaendelea kuelimisha jamii kuachana na tabia ya kuuza mali za familia.
“Hivi sasa vitendo vya wanaume kushinda kwenye vijiwe na migahawa imepungua, kipindi cha nyuma wanashinda vijiweni kuanzia asubuhi, tukapiga marufuku wasikae vijiweni hadi saa 10 jioni ndiyo vinafunguliwa ili asubuhi washiriki shughuli za maendeleo kwa kweli tunaenda vizuri sasa”,amesema Kayange.
“Changamoto iliyopo sasa ni baadhi ya wanaume kutumia mali za familia kutafuta wanawake wanaokuja sentani kujiuza (Nzige) nyakati za mavuno, tunaendelea kudhibiti pia. Bado kuna kuna mfumo dume, mwanamke na mwanaume wanalima pamoja lakini wakati wa mavuno mali zinaonekana ni za mwanaume tu. Mwanamke anaonekana wa kuja tu”,amesema Kayange.
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Happiness Misael amesema kwa Mwamala hawajawahi kukutana na hiyo kesi ya kuwepo kwa wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao.
“Kwa Mwamala hatujapata kesi ya kuwepo kwa ma dada poa. Katika Halmashauri ya Shinyanga tunaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa chakula kwa kushirikiana na maafisa watendaji wa kata.Kwenye maeneo ambayo tunabaini tunashirikiana na maafisa watendaji, huwa tunakutana na madada poa kuhusu mabadiliko ya tabia na masuala ya uchumi. Pamoja na elimu hiyo pia huwa tunawapa huduma za upimaji afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaohusika na makundi maalumu”, amesema Misael.
Social Plugin