JUMLA ya timu 8 kutoka kata mbalimbali za halmashauri ya jiji la Tanga zinawania Ng'ombe mmoja na Kombe katika michuano ya ligi ya Machupa Super Cup zikianzia kwenye hatua ya makundi kumtafuta mbabe wao wakati fainali ikitarajiwa kuchezwa siku ya Boxing Day Desemba 26, 2022.
Utepe wa wa ligi hiyo ulikatwa Desemba 9 , 2022 katika uwanja wa Magomeni timu zinazowania kombe hilo zikiwa zimepatiwa jezi seti moja pamoja na mpira kutoka kwa mdhamini na mdau wa michezo Thomas Machupa huku zenyewe zikichangia kiingilio cha shilingi elfu thelasini.
Wakati bingwa akiondoka na Ng'ombe pamoja Kombe, Mshindi wa pili yeye atapata Jezi seti 1 na mipira miwili tuzo nyingine zikienda kwa Kipa bora,Mchezaji bora, Mfungaji bora, Kiungo bora , Kocha bora na Timu itakayoonyesha nidhamu wakati wote wa michuano hiyo huku mchezaji atakaye tupia Hat-trick akiondoka na mpira wake kwenye hatua ya nusu fainali .
Akizungumza mratibu wa ligi hiyo Erick Mburi 'Nginyo' alisema kuwa lengo la michezo hiyo ni kuinua ari ya michezo kwa vijana kuwaepusha na makundi hatarishi ambayo mara kwa mara wamekuwa wakishukiwa nayo hasa katika kata ya Magomeni wakijipanga kusafisha taswira na mtazamo wa jamii kwa vijana hao.
"Zamani Magomeni ilitengeneza jina la kuwa na vijana wahalifu kila tukio linalofanyika Tanga ni Magomeni lakini kupitia michezo hii itazidi kuisafisha Magomeni mpya na ya sasa, na kwa sasa hivi mambo hayo hayapo tuna imani tutafanya makubwa zaidi kupitia michezo hasa kwa upande wa vijana wetu wanaopenda michezo", alisema.
Nginyo alisema kuwa vijana wengi wanapenda michezo changamoto iliyopo ni uwezeshwaji kutoka katika upande wa fedha na kuanzisha ligi mabalimbali kutoka kwa wadau ambazo zingekuwa ni njia sahihi ya vijana hao kuonesha vipaji vyao walivyo navyo na hatimaye kuwa na wachezaji ambao watasaidia katika timu zinazoshiriki ligi tofauti tofauti ndani na nje ya mkoa wa Tanga.
"Tunamshukuru sana mdau na mdhamini wa ligi hii , Thomas Daffa Machupa kwa kuona hitaji la vijana hasa katika michezo, vijana wengi wapo mtaani wanapenda michezo na wana uwezo mkubwa kama wakiwezeshwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kwamba bado wadau hawajajitokeza kwa wingi kudhamamini na kuanzisha mashindano ambayo pengine yangekuwa ni njia sahihi ya vijana wetu kuonekana mimi niwaombe sana wadau na wapenda michezo kwa ujumla waliopo jiji la Tanga kuliona hilo", aliongeza Nginyo.
Timu hizo nane ambazo zinashiriki mashindano hayo ni Magomeni Star,Duga Fc, Talent Fc , Magomeni United,Jiwe, Madongo,Majengo na Urugwai.
Fainali ya Machupa super cup inatarjiwa kuwa ya kipekee na kutakuwa na mambo mbalimbali ikiwemo kupima Afya,huduma ya chanjo ya korona na kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ili kulinda Afya zao.