Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Jamal Kassim Ali, akimkabidhi tuzo Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (kulia), baada ya kuibuka washindi wa kwanza wa uandaaji wa taarifa za fedha kwa mwaka 2021 katika kundi la Taasisi za Fedha katika hafla ya Tuzo za Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) zilizofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya APC jana tarehe 30 Novemba 2022.
Dar es Salaam 30 Novemba 2022 – Kwa mara ya tatu mfululizo Benki ya CRDB imetunukiwa tuzo ya uwasilishaji wa taarifa bora za fedha kwa upande wa taasisi ya fedha kwa mwaka 2021 na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Tuzo hiyo imetolewa katika mkutano mkuu wa mwaka wa NBAA na hafla ya kuadhimisha miaka 50 ya taasisi hiyo iliyofannyika katika Ukumbi wa Mikutano wa APC Hoteli ulipo Bunju jijinii Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wataalamu nan a wabobezi wa masuala ya uhasibu kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Akikabidhi tuzo hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar, Mheshimiwa Jamal Kassim Ali aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika utayarishaji wa taarifa zake za kifedha jamba ambalo limepelekea benki hiyo kuendelea kuibuka kinara.
Waziri Jamal Kassim Ali alisema kuandaa ripoti za mwaka za Mashirika na Taasisi za Umma kwa viwango vya kimataifa kunazipatia mamlaka za usimamizi, pamoja na wawekezaji na wananchi fursa na uwezo wa kupima ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi husika, kuona namna gani yanawajibika ipasavyo katika kusimamia rasilimali na mikakati ya uendeshaji.
“Tuzo hii hii inadhirisha ni jinsi gani Benki hii imewekeza katika mifumo ya kisasa ya uendeshaji ambayo si tu inaongeza ufanisi bali pia inawezesha wadau wenu kupata taarifa za viwango. Hongereni sana,” alisema Waziri Jamal Kassim Ali huku akizitaka taasisi na mashirika mengine kuiga mfano ambao alisema pia ni ishara ya utawala bora.
Akipokea tuzo hiyo, Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nsekanabo, amesema Benki ya CRDB inatambua umuhimu wa kuandaa taarifa za fedha kupitia mifumo inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.
Alisema kitendo cha kupata tuzo hiyo kwa mara ya tatu mfululizo kunaifanya benki hiyo kuendelea kuongeza jitihada ili kuhakikisha inatoa taarifa zilizobora zaidi.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali hii ni pamoja na kuboresha mifumo yetu ya kukusanya na kuandaa taarifa.
Tumeweza pia kuunganisha mfumo wetu wa utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za fedha (IFRS), hii pia imechangia Benki yetu kuwa bora zaidi,” alisema Nshekanabo.Aidha Nshekanabo alisema kuwa ushindi huo pia unatokana na Benki hiyo kuwa wa mfumo bora wa uongozi unaozingatia misingi ya utawala bora, weledi, uwazi wa taarifa za kifedha, uwajibikaji na kiwango cha juu cha uadilifu wa takwimu.
“Hivi ni vitu ambavyo Mkurugenzi wetu Mtendaji, Abdulmajid Nsekela na sisi kama benki kwa ujumla tumekuwa tukiviwekea mkazo mkubwa,” aliongezea. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, Pius Maneno, alisema Benki ya CRDB imeibuka kinara baada ya kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa na taasisi hiyo kwa zaidi ya asilimia 90.
Kwa mwaka 2022 taasisi zaidi ya 60 zimeshindanishwa katika tuzo hizo zilizo jumuisha vipengele 13.Mwaka 2022 umekuwa wa mafanikio makubwa kwa Benki ya CRDB ambapo mbali na tuzo hiyo ya NBAA, benki hiyo pia imetunukiwa tuzo za Benki Bora Tanzania na majarida maarufu duniani ya fedha na uchumi ya Euromoney na Global Finance.
Social Plugin