Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa akifungua mkutano mkuu maalum wa UTPC, unaofanyika Jijini Dar es salaam
* Waandishi wakongwe watakiwa kuwaelekeza vijana
Na Seif Mangwangi, Dar es salaam
SERIKALI imewataka waandishi wa habari wakongwe kuwaeleza waandishi vijana kuwa uandishi wa habari ni kazi ngumu inayohitaji ubunifu, uadilifu na uvumilivu na sio ujanja ujanja.
Akifungua mkutano Mkuu Maalum wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC), Msemaji na Serikali na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Habari/Maelezo Gerson Msigwa amesema fani ya uandishi wa habari ni ngumu na inahitaji moyo wa ujasiri na ukiwa na Moyo mwepesi watabakia waandishi wajanja wajanja na kupoteza kundi kubwa la waandishi waadilifu.
Wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wakiwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC
Amesema waandishi wakongwe walijengewa nidhamu ya kutosha na mazingira ya kufanya kazi yalikuwa magumu tofauti na sasa.
"Zamani sisi tulikuwa tunafanya kazi kwa ugumu na tulikuwa watiifu na wabunifu, tena bila vifaa, waambieni vijana wetu wawe wabunifu, watumie teknolojia vizuri," amesema.
Amesema vijana waelezwe kuwa uandishi wa habari sio rahisi na bila kufanya hivyo tutabakiwa na waandishi wajanja wajanja na kupoteza waandishi wenye weledi baada ya wao kukata tamaa na kukimbia kufanyakazi zingine.
" Hii haiwezi kuwa kazi rahisi sana sababu tunapigania haki za watu, tunatetea wanyonge na tunatangaza maendeleo, kwa hiyo waelezeni hii ni kazi ngumu na hata kupata maslahi yake ni ngumu," amesema na kuongeza:
"Moja ya changamoto tulizokuwa nazo ni hali ya uchumi, wadau wa maendeleo tunaomba mtusaidie kutukwamua tulipo ili tuweze kufanya kazi zetu vizuri na kwamba kufanya hivyo sio kuwa omba omba, tunataka tubadilike,".
Aidha Msigwa ametoa wito kwa Serikali za Mkoa kuchangia Klabu za waandishi wa habari kwa kuwa wamekuwa nguzo kubwa ya kuhamasisha maendeleo ya Mkoa husika kwa kuhabarisha umma mambo yote yanayoendelea katika Mkoa.
Pia amewataka waandishi wa habari kufanya kazi zao bila uoga wowote lakini kwa kufuata misingi na weledi bila kuvunja sheria za nchi ikiwemo kuandika habari za uongo ambazo matokeo yake ni kuharibu taswira ya nchi.
Hata hivyo Msigwa amevipongeza vyombo vya habari siku za karibuni kuanza kuandika habari kwa weledi bila kufuata taarifa potofu ambazo zimekuwa zikiandikwa mitandaoni na ambazo hazijafanyiwa uchunguzi.
Kuhusu Maslahi bora kwa waandishi wa habari, Msigwa amewataka waandishi wa habari kubwa mabalozi wazuri kwa kuandika habari zenye weledi zitakazovutia wawekezaji kuja nchini kuwekeza na kutoa ajira.
" Najua vyombo vingi vya habari havilipi mishahara hivyo tunatakiwa sisi tujenge mazingira mazuri ambayo yatavutia wawekezaji kuja kuanzisha vyombo vikubwa na kuajiri wenzetu. Takwimu zinaonyesha kila mwaka kuna waandishi wa habari 1000 wanazalishwa nchini, hawa wote wanaenda wapi?,"alihoji Msigwa.
Kuhusu sheria ambazo sio rafiki, Msigwa amesema tayari taratibu mbalimbali za kufanyia mabadiliko hayo zimefanyika na hivi karibuni sheria hiyo itafikishwa bungeni kwaajili ya kufanyiwa mabadiliko.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Rais wa UTPC, Deo Nsokolo amesema kikao hicho maalum kina lengo la kufanyia mabadiliko mfumo mzima wa UTPC na kuitoa kutoka katika kuwa bora na kuwa bora zaidi ( moving from Good to Great) ikiwemo kuhamisha makao makuu kutoka Mwanza na kuhamia Dodoma.
Akitoa salamu za mashirika ambayo ni marafiki na UTPC, Mkurugenzi wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa, amewataka waandishi wa habari kuungana na kwamba siku zote hakuna jambo la muhimu kama usalama wa mwandishi wa habari kwanza.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa UTPC
" Nawaomba ndugu zangu, tuungane ili kuhakikisha sheria iliyopo inabadilishwa kwaajili ya maslahi mapana ya waandishi wa habari, hakuna jambo muhimu zaidi ya usalama wa Mwandishi kwanza," amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Keneth Simbaya amesema mabadiliko yanayoenda kufanyika yanahitaji utayari wa viongozi wote wa klabu na kwa kufanya hivyo wafadhili wataendelea kuipatia fedha UTPC na kuifanya kuwa imara zaidi.
Wajumbe
Social Plugin