Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI DKT. GWAJIMA : KUPINGA UKATILI NI AJENDA YA KITAIFA, UKATILI WA KIJINSIA ASILIMIA 60 UNATOKEA NYUMBANI, 40% SHULENI


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga akiwa ndani ya Studio za Radio Faraja Fm Stereo. Kushoto ni Mtangazaji wa Radio wa Faraja Fm, Simeo Makoba.


Na Moshi Ndugulile - Shinyanga
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema ukatili ni ajenda inayohitaji juhudi za pamoja kupinga vitendo hivyo, kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 60% ya ukatili wa kijinsia kwa Watoto hutokea majumbani wakati asilimia 40% hufanyika shuleni.


Amesema kuwa Mwaka 2021 Watoto 11,499 walifanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kubakwa,kulawitiwa na mimba katika umri mdogo ,hali ambayo inahitaji kuongeza kasi ya kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo ni kikwazo dhidi ya maendeleo na ustawi wa jamii


Dkt.  Gwajima ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Desemba 5,2022 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na viunga vyake kupitia kipindi maalumu cha Redio Faraja Fm, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Dkt Gwajima ameeleza kuwa takwimu za Mwaka 2021 zinaonesha kuwa watoto 5,899 walibakwa,wakati 1,114 walilawitiwa na wengine 1677 walipata mimba katika umri mdogo,vitendo ambavyo watoto wanafanyiwa wakiwa katika mazingira ya nyumbani au shuleni


“Tunajenga shule ili watoto wasome na kuhitimu lakini wanaishia kupata mimba katika umri mdogo, tafiti zinaonyesha vitendo vya ubakaji na ulawiti hutokea nyumbani kwa asilimia 60,na asilimia 40 hutokea shuleni,serikali haitaweza kujenga shule kwa ajili ya kutunza watoto ili waendelee na kustawi katika maisha yao lakini kumbe huko huko wanabakwa,huko huko wanalawitiwa,lakini ulawiti unaanzia nyumbani walipo Baba,Mama,ndugu na jamaa na baadaye unaenea shuleni kwa watoto wengine ambao pengine wazazi wao wanajitahidi kuwalinda lakini wanakuja kushawishiwa wakiwa katika mazingira ya shuleni”, amesema Dkt.  Gwajima.


Amesema suala la kupinga ukatili wa kijinsia na kwa Watoto ni agenda ya kitaifa inayolenga kuwa na taifa lenye maendeleo na ustawi wa jamii ,kwani vitendo hivyo visipodhibitiwa vitakwamisha juhudi za serikali na wadau zinazolenga kutokomeza matukio ya aina hiyo.


Dkt. Gwajima amezitaka kamati zote zilizopo kwenye mfumo unaohusika na mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto,kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ukatili kama sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili ili kuleta tija.


Waziri Dkt. Gwajima amefanya ziara ya siku moja Mkoani Shinyanga ambapo ametembelea shule ya sekondari Town iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga,k uzungumza na wananchi kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kupitia Redio Faraja fm, ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, kutembelea Kamati ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga, lakini pia amekabidhi vyeti vya pongezi kutambua mchango wa baadhi ya taasisi na watu binafsi katika kushiriki mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.


Tanzania imeungana na nchi nyingine Duniani kuadhimisha kampini ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ambayo hufanyika kimataifa Novemba 25 hadi Disemba 10 ya kila Mwaka,ambapo kwa Mwaka huu kauli mbiu inasema “KILA UHAI UNA THAMANI,TOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA NA KWA WATOTO”

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga akiwa ndani ya Studio za Radio Faraja Fm Stereo. Kushoto ni Mtangazaji wa Radio wa Faraja Fm, Simeo Makoba
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga akiwa ndani ya Studio za Radio Faraja Fm Stereo.
Mtangazaji wa Radio wa Faraja Fm, Simeo Makoba (kulia) akimuuliza swali Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ndani ya Studio za Radio Faraja Fm Stereo.  
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga akiwa ndani ya Studio za Radio Faraja Fm Stereo. 
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akisalimiana na Mtangazaji wa Radio wa Faraja Fm, Simeo Makoba baada ya kuwasili Radio Faraja leo Jumatatu Disemba 5,2022.

Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com