Afisa Mtendaji kata ya Mwamala Halmashauri ya Shinyanga, Suzana Kayange
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia inayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kupenya kwenye maeneo mbalimbali wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ambapo sasa wananchi wameanza kuuzika mfumo dume kwa kuhakikisha wanawake wanamiliki mali na kugawana mali pindi wanapotengana na waume zao.
Haya yanajidhihirisha katika kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambako Malunde 1 blog imetembelea eneo hilo na kuzungumza na wakazi wa eneo hilo ambao wanasema sasa mambo yamebadilika jamii imeanza kuachana na mfumo dume unaomfanya mwanamke aonekane si lolote.
“Sasa hivi hakuna kufukuza mwanamke, mkiachana mnagawana pasu kwa pasu, hakuna kunyanyasa mwanamke”,anasema Masesa Masele.
“Sasa tuna elimu ikitokea tumeachana na mme wangu lazima tugawane mali, kila mtu anachukua nguvu zake”,anaongeza Esther Thomas.
Naye Mboje Malale anasema kidogo kidogo jamii imeanza kubadilika kutokana na kelele za kupinga ukatili wa kijinsia.
“Inapotokea mwanamke na mwanaume wakaachana, lazima kuna aliyeanzisha mgogoro hivyo lazima anayeanzisha mgogoro lazima wagawane”,amesema Mzee Malale.
Afisa Mtendaji kata ya Mwamala Halmashauri ya Shinyanga, Suzana Kayange amesema licha ya wananchi kuwa na elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia lakini bado kuna mfumo dume, mfano mwanamke na mwanaume wanalima pamoja lakini wakati wa mavuno mali zinaonekana ni za mwanaume tu, Mwanamke anaonekana wa kuja tu.
“Matukio ya ukatili wa kijinsia yamepungua kwa kiasi kikubwa, kesi zimepungua sana, wanawake hawanyanyaswi mfano kupigwa kama zamani, wanaume wanaogopa kuchukuliwa hatua endapo watabainika kunyanyasa wake zao kwani wananchi wameshajua mahali pa kuripoti matukio ya ukatili, wajane pia sasa wanapata haki zao”,amesema Suzana.
Social Plugin