Wanandoa kutoka India, ambao ni mashabiki wa soka walisherehekea kombe la dunia la mwaka huu kwa kuvalia jezi za Messi na Mbappe wakifunga pingu za maisha kabla ya kukimbilia kutazama fainali.
Sachin na Athira R hawakutaka siku ya harusi yao izuie mapenzi yao kwa soka, na ingawa wanapendana kama chanda na pete hawakubaliani kamwe linapojiri swala la timu ya kuunga mkono.
Gazeti la Malayala Manorama liliripoti kwamba Sachin alikuwa shabiki mkubwa wa nyota wa Argentina Lionel Messi, naye Athira aliiunga mkono timu ya Ufaransa yake Kylian Mbappe.
Waliupenda sana mchezo huo kiasi kwamba hawakuchagua vazi la jadi la harusi na badala yake waliamua kuvaa jezi za soka za Ufaransa na Argentina zenye majina ya Messi na Mbappe.
Saa chache kabla ya timu hizo mbili kukutana katika Uwanja wa Lusail nchini Qatar Jumapili, Desemba 18, walifunga ndoa kwenye sherehe iliyofanyika katika jiji la Kochi, Kerala, India. Walivalia jezi na kujipamba na vito wakati wakafanya harusi yao ya kitamaduni.
Argentina ilishinda fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2, na kumpa Messi mwenye umri wa miaka 35 nafasi ya kunyanyua taji la Kombe la Dunia baada ya kushinda Mpira wa Dhahabu wa Adidas kwa Qatar 2022.
Fainali za Kombe la Dunia za FIFA, zilizochezwa Jumapili, Desemba 18, zimeshuhudia timu shiriki zikiweka mfukoni mabilioni ya fedha kama zawadi. Washindi Argentina waliondoka na $42 milioni (KSh 5.2 bilioni) kama pesa za zawadi baada ya kuwashinda mabingwa watetezi Ufaransa kwenye mikwaju ya penalti.
Ufaransa, ambayo ilimaliza ya pili katika shindano hilo, ilijinyakulia dola milioni 30 (KSh 3.7 bilioni) za pesa za zawadi hiyo. Ni KSh 2.64b pekee FIFA iliweka bajeti ya $440 milioni (KSh 54.2 bilioni) pesa za zawadi kwa washindi wa Kombe la Dunia la 2022, ambayo ilikuwa juu zaidi ya misimu iliyopita. Mnamo 2018, washindi Ufaransa walijishindia $38 milioni (Ksh.4.6 bilioni) kama zawadi, huku mwaka wa 2014, Ujerumani ilijinyakulia dola milioni 35 (Ksh.4.3 bilioni) baada ya kuibuka washindi.
Social Plugin