Wakazi wa
kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali kuongeza
idadi ya watumishi katika zahanati ya Kijiji cha Bugogo yenye mtumishi mmoja (Nesi pekee) na Mwamala B yenye watumishi
wawili tu hali ambayo inasababisha changamoto kwa wananchi wanapokwenda kupata
huduma za matibabu.
Wakizungumza
na Malunde 1 blog kwa nyakati tofauti wakazi wa kata hiyo wamesema upungufu wa
watumishi katika zahanati ya Mwamala B na Bugogo unasababisha wananchi hususani
akina mama na watoto kutumia muda mrefu wakisubiri huduma za matibabu na wakati
mwingine kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu nje ya kata hiyo.
Pia
wameiomba serikali ijenge kituo cha afya au kuongeza huduma kwenye zahanati
zilizopo kama vile huduma za upasuaji ili kuwapunguzia adha akina mama
wajawazito kusafiri hadi Samuye au Shinyanga mjini kufuata huduma za afya pindi
wanapohisi watajifungua kwa njia ya upasuaji.
“Watumishi wa afya hawatoshi, vitanda na vyumba vya kujifungulia kwa akina mama havitoshi,akina mama tunakosa pa kujifungulia, uchungu ukiwahi unajifungulia chini”,ameeleza Bi. Martha Tungu.
Bw. Madale
Nyewe amesema kufuatia changamoto ya upungufu wa watumishi hao wachache waliopo
wanaelemewa na wagonjwa na wakati mwingine
kutofanya kazi siku za Jumamosi na Jumapili, wagonjwa wanalazimika
kwenda Samuye, Nhelegani au Shinyanga mjini kupata huduma za matibabu.
“Kama
daktari ni mmoja, nesi mmoja tu na idadi ya wagonjwa ni wengi mimi naumwa
halafu wakati mwingine hawapo kinachotokea ni nini?... Ukiona hivyo unajiongeza
tu unaenda kupata matibabu Mjini Shinyanga, tunaomba serikali ituongezee
watumishi wa afya”,amesema Bi. Justina Mihayo.
“Tulilomba
bhize bhanesi, bhize Bhaganga, Ihaha Nesi omo doo, Nganga omo doo gede wa bhugota,
yaya lulu (Tunaomba waje manesi, waje waganga, sasa hivi ni nesi mmoja tu,
daktari mmoja tu kama wa dawa, hii si sawa)”,amesema Bi. Kang’wa Cherehani.
“Tunataka
serikali ilete watumishi wa afya kwenye zahanati zetu ili tupate huduma bora…hawa
watumishi waliopo wanafanya kazi zaidi ya uwezo wao, wakati mwingine wanachoka
tu kutokana na idadi kubwa ya wagonjwa, serikali ituhurumie kwa kweli”,ameongeza
Bw. Nkende Mabula na Masesa Masele.
Afisa
Mtendaji wa kata ya Mwamala Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga , Suzana Kayange amesema ni kweli zahanati ya kijiji
cha Mwamala B ina watumishi wawili pekee
na Bugogo yupo mtumishi mmoja baada ya mtumishi mmoja kufariki dunia.
Ameongeza
kuwa kata hiyo yenye zaidi ya wananchi 10,000 kaya zaidi ya 1000 ina vijiji vinne
ambayo ni Bugogo, Mwamala B, Bunonga na Ibanza ambapo katika kijiji cha Bunonga
majengo ya zahanati yapo usawa wa renta, zahanati ya kijiji cha Ibanza majengo
yapo usawa wa madirisha.
“Majengo
haya ya zahanati yamejengwa kwa nguvu za wananchi, tumeiandikia serikali kuu na halmashauri
na wadau watusaidie kumalizia ujenzi wa zahanati hizi ili kuwasogezea huduma za
matibabu wananchi”,amesema Kayange.
“Kutokana na
changamoto hii wananchi wa kijiji cha Ibanza wanaenda Mwamala kupata huduma za matibabu na
wananchi wa kijiji cha Bunonga wanaenda zahanati ya Bugogo. Kulingana na idadi kubwa
ya wananchi watumishi wanahitajika kwa wingi ,wanatakiwa 15 kila zahanati”,ameeleza
Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dkt. Nuru Yunge amekiri kuwepo kwa changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye zahanati nyingi katika halmashauri hiyo.
"Tuna changamoto, kuna zahanati nyingi tu zina mtumishi mmoja mmoja, tunaangalia namna ya kufanya Re- alocation kwa watumishi ndani ya halmashauri. Hiyo zahanati ya Bugogo yenye mtumishi mmoja tutapeleka mtumishi, ni nesi tu yupo pale, daktari alifariki dunia. Sasa hivi tunatafuta kwanza mtumishi wa kupeleka pale zahanati ya Bugogo",amesema Dkt. Yunge.
"Ili kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye zahanati tunachofanya tunaangalia sehemu ambayo ina nafuu, tunapeleka sehemu zenye changamoto kwa sababu hatuna ajira mpya, ajira mpya tulipata watumishi 38 na wengi walipangiwa kwenye hospitali ya wilaya na vile vituo vipya vinavyofunguliwa",ameongeza Dkt. Yunge.
Social Plugin