MKURUGENZI wa Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) Yusuph Nassor amechukua Fomu ya Kuwania Nafasi ya Mwenyekiti wa Klabu ya Simba katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 29 Mwaka 2023 .
Kamati ya Uchaguzi wa Simba ilifungua mlango wa kuchukua fomu Desemba 5 kwa wagombea wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo ya Uenyekiti ambayo kwa Sasa ipo chini ya Murtaza Magungu aliyeuchaguliwa kwenye uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi kujiuzuru.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo Nassor ambaye aliyewahi kuwa MKUU wa Kitengo Cha Fedha ,Utawala na Uendeshaji cha Klabu hiyo amesema ameamua kutumia nafasi yake hiyo ya kikatiba Ili kuingoza Klabu hiyo kongwe baada ya kuona ana kila sababu ya kuhakikisha ana iletea maendeleo.
"Ninaifahamu vizuri Simba kwani mbali ya kuwa kwanza nina mapenzi nayo kwa kipindi kirefu, pia nimefanya nayo kazi vizuri hadi wakati huu nilipoamua kuchukua fomu hii, malengo yangu ni kuiongoza na kuifikisha mbali zaidi kimafanikio" amesema Nassor
Amesema kupitia nafasi mbalimbali za uongozi anazozitumikia na alizowahi kuzitumikia kwa nyakati mbalimbali atahakikisha anaiongoza klabu hiyo na kuipa mafanikio makubwa katika mchezo wa mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.
"Site tunatambua kuwa Simba imepata mafanikio makubwa , malengo yangu ni kuifikisha mbali zaidi kwa kushirikiana na viongozi wenzangu na hiyo ndiyo hasa sababu kuu iliyonifanya nijitokeze kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti" ameongeza Nassor
Simba wanafanya uchaguzi huo baada ya viongozi waliopo madaraka kuongoza kwa miaka minne kwa mujibu wa katiba ambapo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti na wajumbe wanne pekee.
Kwa mujibu wa katiba yao, mwenyekiti atakayechaguliwa ana nafasi ya kuteua wajumbe wawili ambao wataingia kwenye Bodi ya Wakurugenzi wakitimiza idadi ya wajumbe saba kutoka upande wa klabu kuingia katika bodi hiyo.
Social Plugin