Bukindu Bukindu (22), mkazi wa Kijiji cha Ihega, Kata ya Bukoli wilayani Geita amefariki kwa kunywa sumu ya panya siku ya Krismasi, akihofia kudaiwa Sh 45,000 aliyoagizwa kununua vinywaji.
Inaelezwa kuwa kijana huyo amejiua kwa kunywa sumu, baada ya kudaiwa hajalipa shilingi 45,000 ya soda alizokuwa ameagizwa kwenye duka la Masikio ambaye alimpokonya vinywaji na kumsema kwa maneno mabaya.
Shija Antony, ni mama wa marehemu ambapo kwa masikitiko makubwa, ameelezea mazingira yaliyosababisha mwanaye achukue uamuzi huo wa kujiua kwa kunywa sumu.
Ameeleza kuwa mwanaye alipewa fedha kiasi cha shilingi 45,000 na muuza duka mmoja, aliyemtuma kwenda kumnunulia vinywaji kwenye duka la jumla.
Amesema baada ya kufika duka la jumla alilipia na kukabidhiwa vinywaji na alipotaka kuondoka alizuiwa na kuamriwa kurejesha vinywaji na alipoeleza ameshalipia wahusika hawakumuelewa.
Anazidi kueleza kwamba aliporudi kwa bosi aliyemtuma na kumuelezea hali halisi, alimtaka waongozane mpaka kwenye duka hilo la jumla ambapo wauzaji walidai kwamba kijana huyo alikuwa akitaka kuchukua vinywaji bila kulipia.
Licha ya kujitahidi kujitetea, hakuna aliyemwelewa kijana huyo na bosi akamwambia anataka arudishiwe fedha zake na kijana huyo.
Baada ya mabishano hayo, kijana huyo alirudi nyumbani kwao ambapo alichukua maji na kuingia ndani kisha akafunga mlango ambapo muda mfupi baadaye alianza kutapika na ndipo ilipogundulika kwamba alikuwa amekunywa sumu ya panya.
"Ametoka mule ndani na kikombe cha maji akaingia kwake akafunga alivyofunga hivyo nikamsikia anatapika, nikamwambia wewe umefanyaje nikausukuma mlango alikuwa ameurudisha tu, umefanyaje, amenyamaza tu anatapika tu, baadaye katoka nje akawa anatembeatembea tena akaingia ndani akachukua kikombe cha maji akanywa alipomaliza kile kikombe kunywa akarudi ndani akalala akaniambia mama, nilipotoka hapa ilifika nikatumwa na Roba soda kwa Masikio nimefika kule nikampa mke wa Masikio zile hela akanipa soda kwa baadae tena nimetembea hatua mbili akasema hujanilipa hela rudisha hizo soda ndio maana mama nimeamua ninywe sumu sababu na zamani nilimfanyia kazi penyewe siku mbili akanidhulumu", amesema Mama wa kijana huyo.
Hali iliyopelekea wazazi kugoma kuzika mwili wa mtoto wao mpaka watakapojua hatma ya waliosababisha mtoto wao kujiua.
Kaka wa marehemu Yohana Emmanuel anaelezea sababu za wao kugomea kuuzika mwili wa marehemu.
"Tutachukuaje mwili wa marehemu hamjawachukua maelezo sehemu zote mbili, hatujaona yule aliyemtuma kwamba mmemchukua maelezo halafu na kule alikokuwa ametumwa mmechukua maelezo, nimewaambia polisi kwamba sisi hatuwezi tukachukua mwili wa Marehemu na hata kama tukiuchukua inatakiwa tuupeleke kule alipokuwa ametumwa kwenye soda ", amesema Emmanuel.
Jitihada za kumpeleka zahanati kijana huyo aliyehitimu darasa la saba mwaka huu, zilifanyika ambapo alipewa huduma ya kwanza lakini baadaye akafariki dunia.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Ally Kitumbu, amekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza uchunguzi unaendelea kupata kiini halisi cha tukio hilo.
"Hiyo taarifa ya mtoto kunywa sumu tunayo lakini bado tunaichunguza nafikiri ikiwa tayari tutaizungumzia vizuri, niiombe jamii ya mkoa wa Geita na maeneo mengine kwamba kuna mambo ambayo yakikupata unaweza ukatafuta njia sahihi ya kuyatatua badala ya kujiua".
Social Plugin