Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UWEKEZAJI NCHINI WAONGEZEKA TIC YADHIBITISHA


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Ndugu Mathew Mnali ameongea na vyombo vya habari na kusema kuwa miradi iliyosajiliwa katika Kituo Cha Uwekezaji katika kipindi cha Julai hadi Novemba, 2022 imepanda kwa zaidi ya asilimia 22.2 ukilinganisha na kipindi kama hiki mwaka 2021.


Katika taarifa hiyo iliyotolewa katika ukumbi wa mikutano wa Kituo uliopo Mtaa wa Shabani Robert jijini Dar es Salaam leo tarehe 27 Disemba, 2022


Ndg. Mnali amesema kuwa katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2022 Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili jumla ya miradi 132 ikilinganishwa na miradi 108 iliyosajiliwa katika kipindi hicho hicho mwaka 2021.


Amesema kati ya miradi hiyo, miradi ya 50 inamilikiwa na wageni (foreigners) wakati Miradi 30 inamilikiwa na Watanzania (locals) na miradi 52 inamilikiwa kwa ubia kati ya watanzania na wageni (Joint ventures). Miradi hii ina jumla ya thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 3.16 na inatarajiwa kutoa ajira 21,297.


Mnali ameongeza kuwa mgawanyo wa miradi iliyosajiliwa – Kisekta
unaonyesha kuwa Sekta ya Viwanda iliweza kuongoza kwa kuvutia miradi mingi (67), ikifuatiwa na Sekta ya Usafirishaji miradi (25), Utalii miradi (12), Kilimo (9), Huduma (8), Majengo ya Biashara (7), Rasilimaliwatu (3) na Sekta ya Fedha (1).


Aidha, thamani ya miradi (USD bilioni 3.16) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai – Novemba 2022 imeongezeka kwa asilimia 259 ikilinganishwa na thamani ya miradi (USD milioni 881) iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai - Novemba 2021.


Vilevile, kiwango cha ajira kinachaotarajiwa kutokana na miradi iliyosajiliwa Julai – Novemba 2022 kimeongezeka kwa asilimia 57 kutoka ajira 13,578 (Julai – Novemba 2021) hadi ajira 21,297 (Julai - Novemba 2022).


Ongezeko kubwa la Miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji linatokana na Jitihada za Serikali ya Awamu ya sita(6) ya kutangaza fursa mbalimbali za Uwekezaji zilizoko hapa nchini kupitia Ziara mbalimbali za Viongozi wa Kitaifa nje ya nchi pamoja na juhudi kubwa za Serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com