Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWAMALA WALIA CHANGAMOTO YA MAWASILIANO YA SIMU… “SIMU ZINAKATA…TUNASHINDWA HATA KURIPOTI MATUKIO YA UKATILI”


Mfano wa minara ya simu

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Wakazi wa kata ya Mwamala halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wameiomba serikali na Kampuni za Mawasiliano ya Simu kuboresha huduma katika eneo hilo kutokana na kwamba yamekuwa yakisuasua hivyo kusababisha wananchi wakose fursa za mawasiliano wakati mwingine wanashindwa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia yanapotokea.

Wakizungumza na Malunde 1 blog iliyotembelea kata ya Mwamala, wakazi wa eneo hilo wamesema mitandao ya simu imekuwa ikikamata kwa kusuasua sana na kwenye maeneo mengine haikamati kabisa hali inayowafanya kukosa fursa mbalimbali za mawasiliano.

Martha Tungu na Mwajuma John wamesema kukosekana kwa mawasiliano bora kunawafanya wakose fursa za mawasiliano ikiwemo zinazopatikana katika mitandao ya kijamii lakini pia wananchi wamekuwa wakishindwa kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto yanapotokea.

“Ndugu mwandishi wa habari mimi nina simu hii ya mkononi lakini mtandao haukamati kabisa hadi niende pale karibu na ule mti ndiyo Network ishike kwenye hii simu,tunakosa fursa nyingi kutokana na mawasiliano kusuasua, tunaziomba mamlaka zinazohusika ziboreshe mawasiliano katika eneo letu”,amesema Nshoma Samwel.

“Unakuta mwanamke kafanyiwa ukatili usiku wa manane lakini simu haikamati, anashindwa kupata msaada au kutoa taarifa kutokana na simu kutokamata mtandao, tunaomba tuboreshewe mawasiliano ili na sisi tuone dunia ni kiganjani badala ya sasa tupo kama tumetengwa kidigitali”,ameongeza Masesa Masele.

Naye Kang’wa Cherehani amesema mitandao ya simu inasaidia kurahisisha mawasiliano katika jamii hivyo ni vyema Makampuni ya simu yakaendelea kuboresha huduma za mawasilino kwenye maeneo ya pembezoni badala ya kujikita mjini tu.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Wela kijiji cha Mwamala B, Singu Giti Singu anasema ukosefu wa mawasiliano ya simu unaathiri wananchi kwa kukosa fursa zinazotokana na mitandao.

“Tunaomba Makampuni ya simu yaboreshe huduma za mawasiliano, wajenge minara ya simu, kuna matukio mengi yanatokea yana uhitaji wa kupigwa simu ili huduma ipatikane, lakini simu hazipatikani, simu hazikamati mtandao hata kama kuna tukio la ukatili wa kijinsia dhidi ya mwanamke au mtoto linashindwa kuripotiwa. Mawasiliano yangekuwepo ingesaidia kuokoa mambo mengi”,amesema Singu.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwamala Halmashauri ya Shinyanga, Suzana Kayange anakiri kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano akibainisha kuwa ni kubwa kwani mawasiliano ni hafifu, mitandao haikamati hivyo kuwafanya wananchi wakose fursa mbalimbali za mawasiliano.

“Wanawake wanakosa fursa mtandaoni, mitandao inakata kwa kusuasua,hata panapotokea matukio ya ukatili wa kijinsia wananchi wanashindwa kuwasiliana au kutoa taarifa kutokana na changamoto hii ya mawasiliano katika eneo letu”,amesema Kayange.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com