Kiungo wa Yanga Feisal Salum Abdallah (Fei toto) asubuhi ya leo Alhamis Disemba 29, 2022 ameichezea Timu yake ya zamani JKU kwenye mchezo wa Kirafiki dhidi ya Mlandege kwenye Uwanja wa Mao Zedong, Zanzibar ambapo JKU walifanikiwa kupata ushindi wa Mabao 4-2 .
Katika mchezo huo Fei alicheza dakika 45 za kipindi cha pili ambapo wakati anaingia Fei JKU walikuwa tayari wapo nyuma kwa Mabao 2-0, lakini baada ya kuingia wakafanikiwa kusawazisha Mabao hayo na kuongeza mengine mawili huku Fei akifunga moja kati ya Mabao hayo 4 na akiwa na msaada mkubwa wa kupatikana Mabao hayo.
Mwandishi wa Habari hii alifanya jitihada ya kuzungumza na Fei mara baada ya kumalizika mchezo huo lakini Fei aliomba kutozungumza chochote.
“Naomba nisiongee chochote, naomba sana, ikifika siku ya kuongea nitaongea “. Alisema Fei.
Si mara ya kwanza Fei kuonekana kucheza JKU kwani ndio Timu yake ya zamani aliyoondoka mwaka 2018 kabla ya kujiunga na Yanga.
Jumamosi ya Disemba 24, 2022 kupitia mitandao yake ya Kijamii Fei aliwaaga Wanayanga huku timu yake hiyo siku hiyo hiyo ikitoa taarifa yakuwa bado Fei ana mkataba na Yanga mpaka Mei 30, 2024.
Hivi karibuni ziliibuka taarifa ya kuwa Fei huenda akajiunga na Azam FC kutokana na dau nono aliloahidiwa ambapo yeye binafsi aliwahi kusema hachezi mpira kufurahisha Watu bali anacheza Soka kwa kuangalia wapi kuna maslahi.
Social Plugin