Mkazi wa Buseresere wilayani Chato mkoani Geita, Oliva Meshack anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumzika mwanawe wa wiki mbili akiwa hai ili akafanye uchangudoa.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19 anadaiwa kutenda kosa hilo kabla ya majirani kumtilia shaka na kuripoti kituo cha polisi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo amewaeleza waandishi wa habari leo Desemba 15, 2022 kwamba tukio hilo limetokea na lilibainika baada ya majirani kutoa taarifa polisi.
“Jeshi la polisi lilipata taarifa kwa wananchi kuwa kuna binti aliyejifungua lakini wana siku tatu hawamuoni binti na mtoto na wakataka kujua alikopeleka mtoto, tulimchukua binti na kumhoji na alikiri alikuwa ana mtoto wa wiki mbili,” amesema.
Kamanda amesema polisi walipomtaka awaonyeshe mtoto, alidai kutokana na kazi anayofanya alilazimika kumzika ili aweze kuendelea na kazi yake.
“Huyu binti anafanya kazi ya kuuza baa na kuuza mwili wake kutokana na kazi yake mtoto alikuwa kero na anashindwa kufanya biashara zake, akaamua kuchimba shimo na kumzika mtoto akiwa hai,” amesema kamanda huyo.
Amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na jeshi la zimamoto na uokoaji waliongozana na binti huyo hadi alipomzika mwanae na walipofukua shimo walikuta tayari mtoto amekufa.
“Mfumo wake ni kuuza baa na kuuza mwili, unapojitoa kuuza mwili inamaana ushajitoa maisha yako na ndio maana haikushangaza yeye kuzika mtoto. Huu ni ukatili, tuwasihi jamii unapoona binti anaishi maisha ambayo hayampendezi Mungu na maisha yasiyopendeza jamii na yapo kinyume na sheria za nchi, toa taarifa asaidiwe, ashauriwe, anaweza kubadilika na kuwa mtu mzuri,” amesema Jongo.
Pia, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuwaelimisha mabinti hasa wanaoibukia na kuwa na vitendo vya ajabu kutovichukulia kirahisi kwa kuwa vimekuwa vikiwapoteza mabinti wengi