Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MFANYABIASHARA WA M-PESA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA MAJAMBAZI


Mwanaume mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliomvamia usiku katika daka lake katika katika soko la Khayega eneo bunge la Shinyalu kaunti ya Kakamega nchini Kenya.

Majambazi watatu waliojihami kwa silaha kali walimvamia Kevin Orata katika duka lake la M-Pesa usiku wa Jumatatu - Disemba 26,2022 na kutekeleza unyama huo. 

Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kakamega Mashariki Robert Makau alisema kuwa Orata aliyekuwa na umri wa miaka 23 alipigwa risasi na kuaga dunia papo hapo.

Ripoti zinasema kuwa majambazi hao walishuka kutoka kwa pikipiki mwendo wa saa mbili usiku na kuelekea katika duka la M-Pesa karibu na kituo cha mafuta kwenye barabara kuu ya Kakamega kuelekea Kisumu.

Watatu hao kisha walimwamuru mwanaume huyo kuwapa pesa alizokuwa amepata katika biashara hiyo siku hiyo. 

“Waliamuru Orata na mwajiri wake kuwapa pesa na simu zilizokuwa kwenye duka hilo. Alipokataa, mmoja wa majambazi aliyekuwa na bunduki aina ya AK47 alimpiga risasi na kumuua papo hapo,” raia mmoja aliyeshuhudia aliambia waandishi wa habari.

 Genge hilo kisha liliiba kwa haraka kiasi cha pesa kisichojulikana kabla ya kutoroka eneo la tukio kwa kutumia pikipiki. Makau anasema kuwa msako wa kuwatia mbaroni washukiwa hao umeanza.

Chanzo -Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com