Na Mwandishi wetu
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia katika historia kubwa katika nchi hii kwa moyo wake thabiti wa kuipaisha Tanzania kiuchumi na kimiundombinu.
Uthubutu wake Dkt. Samia wa kujenga nchi kiuchumi na kimiundombinu umeendelea kuwagusa Wana Pwani baada ya kusikia kilio chao cha muda mrefu cha kujengwa kwa barabara ambayo itaanzia Utete - Mtemela - Vikumburu - Maneromango - Mzenga - Mlandizi - kuelekea Chalinze.
Rais Samia alitangaza ujenzi wa barabara hiyo Desemba 22, mwaka 2022 kwenye uzinduzi wa kuanza ujazaji wa maji kwenye Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere(JNHPP) kwenye Mto Rufiji mkoani Pwani.
Hatua hiyo inajibu ombi la Mbunge wa Kisarawe Mhe. Dkt. Selemani Jafo, Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Alhaj Abubakari Kunenge ambao wamekuwa wakiomba serikali kujenga barabara inayounganisha Mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara na Mikoa ya Kaskazini ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa kupitia Mkoa wa Pwani bila ya kupitia Mkoa wa Dar es salaam ili kupunguza msongamano na kufupisha muda wa safari kwa wanaokwenda mikoa hiyo sambamba na kuimarisha uchumi na sekta ya utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Bwawa la Nyerere.
Hakika barabara hii itakuwa mbadala hata kwa wananchi wanaoingia jijini Dar es salaam kwakuwa kwasasa Serikali inaendelea na ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Kisarawe Mjini kwenda Maneromango.
Ujenzi huu unaendelea eneo la Kijiji cha Sungwi hivyo mwananchi anayetoka Mikoa ya kusini anaweza kukwepa foleni ya maeneo ya Vikindu na Mbagala anaweza kupitia Utete - Kisarawe Mjini na kuingia katika Jiji la kibiashara la Dar es salaam ndani ya muda mfupi.
Ni wazi barabara hii itaing'arisha Pwani kiuchumi na kuongeza mchango mkubwa kwa pato la Taifa. Hakika huu ni ukombozi mkubwa sana kwa Tanzania na wananchi wote wa Mkoa wa Pwani.
Hongera sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Hakika Dua na Maombi ya wana -Pwani yapo kwako Mhe.Rais Samia
Social Plugin