CHUO CHA LGTI-HOMBOLO KIMETOA MAFUNZO KWA VIONGOZI WA CCM DODOMA

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Serikali za mitaa-Hombolo  Dkt.Lameck Mashala.


Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

CHUO cha Serikali za mitaa-Hombolo (LGTI) Jijini hapa kimetoa mafunzo kwa Viongozi wa chama cha Mapinduzi(CCM)ngazi ya wilaya ya Dodoma mjini kuhusu kuboresha utendaji wa kazi hali itakayoondoa muingiliano wa madaraka na kuboresha utendaji kazi.

Hatua hiyo imekuja baada ya hivi karibuni  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI Ramadhan Kailima kukiagiza Chuo hicho kurudisha utaratibu wa kutoa mafunzo kwa madiwani na viongozi wengine pindi wanapochaguliwa ili kuondoa migogoro baina ya viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa chama.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo jijini hapa, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Chama Mapinduzi Taifa(NEC)Donald Mejeti amewataka viongozi hao wa CCM kuwa watiifu na wasimamizi wazuri wa mali za umma ikiwa ni pamoja na kuhoji pale ambapo wanaona haki za wananchi zinaminywa.

Amesema kwa Sasa ilani ya CCM ndiyo inayotekelezwa hivyo Viongozi hao wanapaswa kuelewa kuwa wao ndiyo wasimamizi wakuu wa ilani kwa vitendo.

"Chuo hiki cha Serikali Hombolo ni Cha Serikali na kimetekeleza ilani ya CCM Kwa kuwa ndiyo kinaongoza nchi kwa sasa hivyo wakaona watuongezee elimu ya utekelezaji wa Ilani,"amesema Mejeti.

Amesema viongozi hao wanapaswa kuwasaidia wananchi ili kutoa nafasi kwao kuwa na imani na chama hicho na kuongeza kuwa hiyo ndiyo itakuwa tiketi ya ushindi wa kishindo wakati wa uchaguzi.

"Mko hapa ili kujifunza uwajibikaji wa majukumu yenu hivyo basi mkafungue milango wananchi wakiona kule kwenye serikali za mitaa kuna urasimu waje kwenu na nyie pia mnaruhusiwa kwenda kwenye ofisi za watendaji wa Serikali kuelezea matatizo ya wananchi na kuyatatua hiyo itasaidia kuwa karibu na wananchi,"amesema.

Mejeti pia ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi hao kutumia vizuri mada zitakazofundishwa katika mafunzo hayo ikiwemo ya ujasiriamali ili kutengeneza uchumi wao.

"Nimeona kwenye ratiba kuna mada ya ujasiriamali nendeni makatengeneze uchumi kwasababu huwezi kutatua shida ya mtu kama hauna kitu mfukoni na ili tuwe sehemu ya kutenda haki lazima tutengeneze uchumi wetu kwanza,"amesema.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo hicho,Dkt.Lameck Mashala amesema lengo la mafunzo hayo ni kutekeleza agizo la Serikali katika kutaka kutoa elimu kwa viongozi kuhusu namna ya kuuishi uongozi na kwamba hatua hiyo  ni mchango wa mamlaka za Serikali za mitaa katika kufikia dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.

Amesema LGTI  kimewajibika kutoa mafunzo hayo ili kushiriki juhudi za Serikali kwenye malengo makuu ya kitaifa ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu ilani ya chama cha mapinduzi kwa vitendo.

Awali akizungumza kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma mjini,Charles Mamba,amesema kuwa mafunzo hayo ni ya Viongozi wa CCM wa Wilaya yote ya Dodoma Mjini yenye Kata 41.

"Niwaombe Mkitoka hapa mkawe wazungumzaji wazuri na mtakayoyapata hapa mkawaelekeze wenzenu wa chini,"amesema Mamba.

Aidha semina hiyo imelenga kuboresha masuala ya uongozi kupitia mada nne ikiwemo ya uongozi ,siasa na itikadi,utekelezaji wa ilani ya CCM, uandishi wa Muhtasari na utunzaji wa kumbukumbu pamoja na ujasiliamali na uhusiano wa uongozi..

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post