Na Isaac Masengwa - Masengwa Blog
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria limemchagua Mch. Dkt. Yohana Ernest Nzelu kuwa Askofu wa pili wa Dayosisi hiyo baada ya kufanya uchaguzi katika mkutano mkuu wa Dayosisi uliofanyika Desemba 9-10, 2022 katika usharika wa Tumaini Bariadi mkoani Simiyu.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mkuu wa Kanisa hilo Dkt. Fredrick Shoo ambapo kwa mujibu wa katiba ya KKKT DKMZV majina yaliyopendekezwa na kupelekwa mbele ya mkutano mkuu Kwa ajili ya nafasi hiyo yalikuwa majina ya wachungaji watatu, Mchungaji Jackson Maganga, Mchungaji Dkt. Daniel Mono na Mchungaji Dkt. Yohana Ernest Nzelu.
Dkt. Yohana Ernest Nzelu alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 187 kati ya kura 244 za wajumbe wa mkutano mkuu wa Dayosisi hiyo walioshiriki mkutano huo. Nafasi ya pili ilienda kwa Mchungaji Daniel Mono aliyepata kura 31 huku Mchungaji Jackson Maganga akipata kura 26.
Askofu Mteule Mch. Dk. Yohana Ernest Nzelu ambaye alizaliwa tarehe 15 Novemba 1974 Kiomboi Mkoa wa singida ataanza kukalia kiti hicho kutoka kwa mtangulizi wake Askofu Dkt. Emmanuel Joseph Makala, baada ya kusimikwa kuwa Askofu kwa ibada maalum ambayo kwa mujibu wa katiba inapaswa kuwa ndani ya miezi sita tangu kuchaguliwa kwake
Dkt. Yohana Ernest Nzelu kama mwalimu wa shule kwa taaluma anachukua kiti cha uongozi wa Dayosisi hiyo inayotimiza miaka 10 tangu kuzaliwa kwake tarehe 12/12/2012 saa 12:00 jioni kukiwa na matarajio makubwa ya kufuata nyayo za mtangulizi wake Dkt. Emmanuel Joseph Makala ambaye ameipa mafanikio makubwa dayosisi katika katika kipindi chake Cha miaka kumi Kwa kazi kazi za utume wa kuinjilisha katika Dayosisi iliyopo mikoa ya Shinyanga na Simiyu ambapo kuna kazi kubwa ya umisionari.
Dkt. Yohana Ernest Nzelu katika utumishi wake kwa mara ya kwanza alifanya kazi katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria akiwa kama mratibu wa Maendeleo ya Jamii na miradi mwaka 1999 na baadaye alibarikiwa kuwa Mchungaji mnamo Septemba 18, 2005 na alitumikia nafasi hiyo katika sharika mbalimbali zilizopo Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria na baadaye Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria
Pia mteule huyo akiwa mkuu wa Shule ya Sekondari Mwadui ametumika kama Mkuu wa majimbo mbalimbali ya Dayosisi hiyo kwa zaidi ya miaka 11.
Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi ya Kiomboi Hospitali mwaka 1984 - 1990 na baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari Minaki iliyopo katika mkoa wa Pwani.
Dkt. Yohana Ernest Nzelu kitaaluma ni mwalimu, Mchungaji na pia ni Doctor of Ministry in Theology aliyosoma kiomboi hospital , Tumaini university kituo Cha mwika, baadae Stefano Moshi memorial university Moshi.
Baadaye akajiunga na Chuo kikuu huria Cha Tanzania ambacho bado anasoma mpaka leo. Pia amesoma Masters na Doctorate ( shahada ya udaktari katika huduma) huko Forty Wayne Marekani
Hadi anachaguliwa kuwa Askofu Mteule Mch. Dkt. Yohana Ernest Nzelu alikuwa ni msaidizi wa Askofu KKKT DAYOSISI KUSINI MASHARIKI YA ZIWA VICTORIA alipochaguliwa na mkutano mkuu wa Dayosisi hiyo mwaka 2020 akichukua nafasi hiyo baada ya mtangulizi wake Mchungaji Trafaina Assery Nkya kustaafu
Alifunga ndoa na Lilian Nzelu Desemba 19, 1999 na wamejaliwa kupata watoto watano, ambao ni Agness Nzelu, Doricas Nzelu, Elizabeth Nzelu, Noel Nzelu na Suzan Nzelu
Pia katika mkutano mkuu huo, waumini wa Kanisa hilo walimchagua Dkt. Daniel Mono kuwa Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi baada ya mtangulizi wake kuchukua nafasi ya uaskofu.
Masengwa Blog iliongea na baadhi ya waumini kupata kufahamu wamepokeaje kuchaguliwa kwake Askofu mteule Dkt. Yohana Ernest Nzelu.
Ibrahim Lyanga kama msharika wa Dayosisi hiyo yeye binafsi amesema ameridhishwa na maamuzi ya mkutano mkuu kwani anamfahamu vyema Dkt. Yohana Ernest Nzelu.
"Mimi binafsi namfahamu Mchg Nzelu kama mtu ambaye ni mwaminifu, mtulivu na msikivu, ni mchg makini sana anayefanya kazi zake kwa kufuata utaratibu. Ana sikiliza vizuri maoni na changamoto za wengine ili kuwasaidia" ,alisema Lyanga.
"Kwa kipindi akiwa mkuu wa shule ya sekondari Mwadui na ameisaidia shule hata kuongeza ufaulu na idadi ya wanafunzi na miundombinu ya shule kuwa bora sana. Ameisaidia kukua na kuimarika kwa majimbo mbalimbali aliyoyaongoza likiwemo Jimbo la Shinyanga, Jimbo la kusini Kati, Jimbo la kusini Mashariki mhunze na Jimbo la Maswa ambayo hayo nilifanya naye kazi akiwa mkuu wangu wa Jimbo 2018 - 2020." ,aliongeza Lyanga ambaye pia ni Katibu/Mtunza hazina wa Jimbo la Shinyanga la Dayosisi hiyo .
Social Plugin