NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na IAS Regional Federal (MENA and Africa) imezindua kiliniki ya uchunguzi na matibabu ya ugonjwa unaosabisha wingi wa mafuta kwenye damu (Lipid clinic) ikiwa ni ya kwanza Tanzania na ya nne Barani Afrika kwa kutoa huduma hizi.
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kliniki hii itakuwa ikifuatiliwa kimataifa na kwamba kwa Afrika pia zipo Sudan, Ethiopia na Somalia.
Kwa mujibu wa Prof. Janabi huduma ya kliniki hii itakua mara tatu kwa wiki kwa upande wa watu wazima na watoto na kuongeza kuwa itasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa kwenda nje ya nchi kupata huduma ambazo awali hazikuwepo nchini.
“Faida za kuingia katika mtandao huu wa hizi kliniki za mafuta, madaktari wetu wawili wa kwanza wataenda kuongeza ujuzi nchini Uingereza katika kutibu haya magonjwa hivyo ni kliniki ambayo itatusaidia kama nchi kwasababu gharama zake ni kubwa takwimu zinaonesha kuwa asilimia 31 ya vifo duniani inahusishwa na magojwa ya moyo” Prof. Janabi
Akizungumza kwa njia ya mtandao wakati wa uzinduzi huo, Rais wa mtandao wa kliniki za magonjwa hayo kutoka Iraq Dkt. Mutaz Al-Sabah amesema wataendelea kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa lengo la kuimarisha kliniki hiyo na kuwajengea uwezo wa wataalamu ili iwe endelevu.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka MNH-Mloganzila, Dkt. Rosemary Minja amesema ili mtu kubainika ana ugonjwa wa wingi wa mafuta kwenye damu ni lazima afanyiwe vipimo na baadaye aweze kupata matibabu.
“Si lazima mtu mwenye ugonjwa huu awe na ugonjwa wa moyo au kisukari wakati mwingine hata watu wenye uzito wa juu au matatizo ya ngozi wanaweza kuwa na ugonjwa huu” amesema Dkt. Minja.
Ameeleza sababu za ugonjwa huu ni pamoja na mtindo wa maisha kwa watu kutofanya mazoezi na kutokula mlo kamili na hivyo ameishauri jamii kufanya mazoezi na kula vyakula kadiri wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya.
Social Plugin