*********************
Na Mwandishi Wetu
Ili kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma za kifedha kwa njia ya vifaa vya Mawasiliano hasa Mawasiliano ya simu; Tanzania itahakikisha inatekeleza usambazaji wa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kuwafikia wananchi wote katika ngazi za Mkoa, Wilaya na vijiji ili kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania wanapata huduma za Mtandao wa intaneti ifikapo 2025.
Aidha, ili kukuza dhana na Utekelezaji wa uchumi shirikishi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, Serikali itaendelea kuziunganisha nchi zinazopakana na Tanzania kwenye huduma za mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alieleza hayo katika Taarifa yake kwa umma katika kuadhimisha miaka 45 ya kuasisiwa kwa shirika la Mawasiliano Afrika ATU.
“Tunaendelea na kazi ya kuunganisha mikoa yote na wilaya zote za Tanzania kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) ambapo hadi sasa tumekamilisha Ujenzi wa Mkongo kwa takribani Kilomita 8,319, lengo likiwa kuunganisha mikoa, wilaya na maeneo yote ya mipaka ya nchi zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Mozambique na Malawi,” alieleza Nape kwenye Taarifa hiyo.
Waziri Nape alibainisha kuwa kazi ya kuunganisha mikoa yote kwenye Mkongo imekamilika na sasa Wizara inafanya kazi ya kuhakikisha huduma za Mkongo huo unaorahisisha Mawasiliano hasa ya intaneti zinaunganisha wilaya zote nchini ili wananchi wanufaike na huduma za kifedha kwa njia ya Mtandao kupitia huduma za mkongo.
“Ili kuhakikisha lengo la ufikiwaji wa huduma za Mtandao hasa wa intaneti linakuwa halisi na kamilifu,uimarishaji na Ujenzi wa miundombinu thabiti na ya uhakika ya Mawasiliano hasa Mawasiliano ya intaneti ni muhimu,” aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari katika Taarifa yake kuadhimisha siku hiyo alieleza kuwa TCRA kama msimamizi wa huduma za Mawasiliano nchini, imejidhatiti kuhakikisha upatikanaji wa huduma za Mawasiliano nchini unakuwa wa uhakika na unaowawezesha wananchi wengi kushiriki kwenye uchumi wa Kidijitali.
Social Plugin