Na Dotto Kwilasa,Malunde 1Blog-DODOMA.
ZIKIWA zimesalia siku chache Tanzania kuadhimisha miaka 61 ya uhuru wake,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru mwaka huu zitumike kujenga mabweni katika shule nane za Msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum hapa nchini.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa kuhusu Maadhimisho ya Sherehe za miaka 61 ya uhuru wa Tanzania Bara.
Amesema Rais Samia ameamua fedha zote kiasi cha Shilingi Milioni 960 zilizokuwa zimetengwa na Wizara na Taasisi kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru mwaka huu 2022,zipelekwe Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili zitumike kuwahudumia wenye mahitaji.
Simbachawene ameeleza kuwa Tanzania Bara ilipata Uhuru wake tarehe 09
Desemba, 1961 na tarehe 09 Desemba, 1962 ikawa rasmi Jamhuri hivyo kila mwaka Tanzania Bara husheherekea Maadhimisho ya uhuru ambapo kwa mwaka huu yataazimishwa kwa kaulimbiu isemayo"Miaka 61 ya Uhuru:"amani na umoja ni nguzo ya maendeleo yetu".
"Kauli mbiu hii inaonyesha nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha uchumi unaojikita katika maendeleo ya watu kwa kufanya mabadiliko katika sekta zote za kiuchumi na kijamii ili kufikisha neema na Maendeleo kwa Wananchi wote wa Tanzania,"amesema Simbachawene.
Simbachawene pia "ameeleza namna yatakavyofanyika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 2022 kuwa ni kwa Midahalo na Makongamano mbalimbali yatakayofanyika katika Wilaya zote hapa nchini kujadili, kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea kuhusu Maendeleo Endelevu ambayo Nchi yetu adhimu Tanzania imeyafikia"amesema.
"Kwa muktadha huu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameniagiza nishirikiane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI kufanya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya Midahalo na Makongamano hayo ili kujiridhisha na matokeo yake hivyo katika kutekeleza maelekezo haya ofisi hizi zimetoa Maelekezo mahsusi na ratiba kwa ajili ya kurahisisha uendeshaji mzuri wa shughuli kwa Mikoa na Wilaya zote nchini,"amesema.
Amesema kuwa Katika kukuza uzalendo na kusherehekea Maadhimisho hayo pamoja na maadhimisho mengine ya Kitaifa kama vile sherehe za Muungano, Ofisi zote za Serikali hapa nchini zipambwe kwa mapambo ya rangi za Bendera ya Taifa pamoja na picha ya Rais.
Social Plugin