Mgeni rasmi Mhe. George Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) akisikiliza maelezo kuhusu Kozi mtandaoni ya Stadi za Maisha, VVU/UKIMWI na Jinsia kwa vyuo vya elimu ya juu na kati.
30 Novemba 2022, Lindi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kwa kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imezindua kozi ya elimu ya stadi za maisha inayolenga Afya ya Uzazi, VVU/UKIMWI na elimu ya kuzuia ukatili wa kijinsia kupitia mtandao, kwaajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati.
Uzinduzi huu umefanyika tarehe 30 Novemba 2022 uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, kwenye wiki ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani katika Kilele cha siku ya Vijana.
UNESCO kwa kupitia mradi wake wa “Haki zetu, Maisha Yetu, Mustakabali wetu” maarufu kama O3 Plus unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la kimataifa la Sweden (SIDA) na mpango wa kudhibiti VVU wa Umoja wa Mataifa (UN Joint program on AIDS), inalenga kuhakikisha kwamba vijana waliopo kwenye vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati nchini Tanzania wanapata matokeo chanya ya afya, elimu, na usawa wa kijinsia kwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU, mimba zisizotarajiwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwakuzingatia hili UNESCO inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza utoaji wa elimu ya stadi za maisha kwa kuzingatia umri, utamaduni na maadili kwenye suala la elimu ya afya ya uzazi kwa kina katika Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya kati.
Kama sehemu ya mpango huu, UNESCO ikishirikiana na mashirika ya Umoja wa mataifa ya UNAIDS, UNFPA na ILO pamoja na Wizara husika (Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya) na Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) vikiwemo pia vyuo vikuu (Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Chuo kikuu cha Iringa, Chuo kikuu cha Mt. Augustine na Chuo kikuu cha Dodoma) ilitengeneza kozi hii inayoweza kusomwa mtandaoni kupitia mfumo wa tehama wa chuo husika au simu ya mkononi. Kozi hii ilifanyiwa majaribio katika vyuo vikuu vinne (UDSM, SAUT, UoI na MUCE) mwaka 2021 ambapo zaidi ya wanafunzi 17,000 walijisajili na kusoma kozi hiyo.
Kwa kupitia majaribio haya, UNESCO ilipata mapendekezo muhimu ya kuzingatia katika kuboresha wa maudhui na mtindo wa uwasilishaji wa kozi kupitia mifumo ya tehama ya kujifunzia vyuoni. Michakato ya kuboresha kozi ilifanyika na kupelekea maboresho yaliyopendekezwa kufanyika kwa wakati.
Uzinduzi wa kozi ya mtandaoni ya elimu ya afya ya uzazi kwa kina inayozingatia stadi za maisha ni hatua muhimu ya kuboresha mazingira salama ya kujifunzia na kufundishia kwa Wanafunzi na Walimu wa Taasisi za elimu ya juu na kati. Wanafunzi watakaosoma kozi hii watapata uelewa na kujenga umahiri wa kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza kwenye maisha yao wawapo vyuoni na hata baada ya kumaliza masomo hususani kwenye masuala ya VVU/UKIMWI, afya ya uzazi, jamii na uchumi.
Pia kijana atakayesoma kozi hii ataweza kufurahia maisha yake ya chuo na kuweza kufikia malengo yake ya elimu na kuweza kuchangia kwa ufanisi zaidi katika maendeleo ya nchi kama mhitimu wa elimu ya juu na kiongozi wa baadae.
Kozi hii imetengenezwa kwa maudhui na mtindo wa kuvutia ili kuwawezesha wanafunzi kuisoma kwa wepesi wakati wowote, mahali popote kwa ratiba yao wenyewe.
Katika kuchangia mipango ya Kitaifa ya sekta ya VVU/UKIMWI pamoja na Afya, baada ya kuzindua kozi hii TACAIDS kwa kushirikiana na wizara na wadau itaisambaza kwenye Vyuo vyote vya elimu ya juu na elimu ya kati nchini.
UNESCO katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kama moja ya lengo la maendeleo endelevu inashirikiana na wadau wa elimu kuweka mazingira salama na jumuishi ya kusomea kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu na elimu ya kati wa Tanzania, ili kufanikisha wanafunzi kumaliza safari yao ya elimu bila vikwazo.
Social Plugin