Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba akizungumza na wakandarasi wakati wa hafla ya kusaini mikataba ya Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu ambao utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga yenye thamani ya shilingi bilioni 76.9 tarehe 19 Desemba, 2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam. Mkurugenzi Mkuu wa REA Mha. Hassan Saidy akizungumza na Wakandarasi wakati wa hafla kusaini mikataba ya Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu ambao utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga yenye thamani ya shilingi bilioni 76.9 tarehe 19 Desemba, 2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam. Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na REA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nishati wakati wa Hafla ya kusaini mikataba ya Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu ambao utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga yenye thamani ya shilingi bilioni 76.9 tarehe 19 Desemba, 2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam. Wakandarasi wa Kampuni ya DIEYNEM CO LTD Mkurugenzi Mkuu Maulid Ngaiwa wa pili kushoto na Katibu wa Kampuni Novatus Lyimo wakishuhudia wakati Mkurugenzi Mkuu REA Mha. Hassan Saidy akisaini Mkataba na kampuni hiyo katika hafla ya kusaini mikataba ya Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu kwa wakandarasi mbalimbali walioshinda zabuni ambao utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga yenye thamani ya shilingi bilioni 76.9 tarehe 19 Desemba, 2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam.
**********************
Na Dorina G. Makaya – Dar-es-salaam
*vijiji vyote nchini vitakuwa vimefikiwa na umeme kabla ya mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 19 Desemba, 2022 na Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alipokuwa akizungumza na Wakandarasi katika hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa Mradi wa Peri Urban III kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakandarasi iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar-es-salaam.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa hiyo ni ahadi ya uhakika ya Serikali na kuwa Serikali itahakikisha umeme unapelekwa kwenye maeneo yote ya uzalishaji mali, utoaji huduma za Afya, zahanati, pump za maji na viwanda vya kusagia mazao.
Leo hii ni siku ya kusaini mikataba ya Peri Urban yenye thamani ya shilingi bilioni 76.9 kwa ajili ya kupeleka umeme pembezoni mwa miji kwenye baadhi ya mikoa kwani miji inapanuka na kuna maeneo pembeni mwa mikoa hayana umeme. Alisema Waziri Makamba.
Ameongeza kuwa, uongozi mzima wa Wizara ya Nishati umeshiriki katika hafla hiyo ikiwa ni ishara kuwa, jambo hili limechukuliwa kwa uzito wa kipekee lakini pia ni ishara inayoonyesha kwamba sasa Wizara ya Nishati imeamua kufanya kazi hii ya kupeleka umeme vijijini, vitongojini na pembezoni mwa miji kwa namna mpya.
Amesema uongozi mzima wa Wizara ya Nishati, sasa utajielekeza upya kwenye miradi ya REA baada ya kubaini kusua sua kwa utekelezaji wa baadhi ya Miradi ya kupeleka umeme vijijini.
Waziri Makamba ameeleza zaidi kuwa, fedha nyingi sana za Serikali na za Washirika wa Maendeleo, zinatumika katika kutafuta Wakandarasi kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo ambayo watu wanauhitaji wa umeme lakini wananchi katika maeneo hayo, hawaoni kasi wanayoitarajia.
Amesema, Katika maeneo mengi wanaona wananchi wanaona wakandarasi wamesimika nguzo wameondoka, wengine wameweka waya wameondoka, wengine wamepima wameondoka na inachukua muda mrefu sana kukamilisha miradi hii.
Waziri Makamba ameeleza kwa hisia kuwa, kama Serikali, jambo hili linaikera Serikali. Na kukumbushia kuwa, Ilani ya Chama cha tawala imetoa maelekezo mahsusi kuhusu kufikisha umeme vijijini.
Makamba amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa maelekezo mahsusi kwamba vijiji vyote hapa nchini vifikiwe na umeme kwa wakati lakini utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya chama tawala na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kidogo kasi yake si ya kuridhisha.
Amesema katika mkutano mkuu wa chama tawala, michango iliyotolewa kuhusu taarifa ya Serikali, kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara iliyopewa nafasi ya kuchangia mikoa 19 iliongelea umeme vijijini.
“Hatuwezi kuendelea hivi. Lazima tubadilishe utaratibu wa usimamizi wa Miradi hii. Haiwezekani, jambo linasua sua alafu wewe hubadilishi wala hushtuki kuhusu namna ya kulifanya tofauti. Sasa kuna mambo kadhaa ambayo tutayafanya. Mengine tutawachia bodi na Menejimenti waende wakakae na kuyatafakari namna bora zaidi ya uharakishaji miradi ya kupeleka umeme vijijini. Alisema Waziri Makamba.
Waziri Makamba amesema, moja ya mambo ambayo Serikali itafanya ni kuwa, itaajiri waratibu wa Miradi ya REA, vijana 130 kwenye kila Wilaya ambao, watakuwa wanakaa huko huko kwenye maeneo ya miradi.
Amesema, kila wilaya kuanzia sasa, itakuwa na mtu mahususi kwani kwa sasa REA hawana watumishi kwenye mikoa na wilaya hivyo, REA itakuwa na watumishi wake kila mkoa na kila wilaya ambapo watafanya kazi kila siku kwa kutumia usafiri wa pikipiki, baiskeli, na bajaji na watakuwa katika maeneo ya mradi wakiwasimamia wakandarasi na kutoa taarifa wizarani, na kwa viongozi wengine kwenye ngazi ya wilaya kuhusu maendeleo ya miradi. “Hivyo, iwapo mkandarasi amechelewa kuleta waya au nguzo tutajua siku hiyo hiyo hatutangoja mambo yakichelewa.” Alisema Makamba.
Waziri Makamba ameongeza kuwa, Wizara itaweka mfumo wa mawasiliano kati ya waratibu na Wizara ili Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu waweze kupata taarifa ndani ya siku moja kujua nini kinaendelea katika maeneo yote ya mradi na itaiwezesha Wizara kuwa na taarifa zote kiganjani.
Waziri Makamba ameeleza zaidi kuwa, tayari kibali cha kuajiri watumishi hao kimepatikana na baada ya krismasi kutakuwa na usaili ambapo mwaka mpya matokeo yatatangazwa na kila mhusika atajua wilaya yake.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa anaamini hatua hiyo itasaidia katika kuharakisha usimamizi wa miradi hiyo.
Akitoa maelekezo kwa wakandarasi waliofanikiwa kupata mikataba ya kutekeleza miradi ya REA, amesema, kumekuwa na baadhi ya wakandarasi ambao baada ya kupata miradi wamekua wakisua sua katika utekelezaji wa miradi ya REA waliyokabidhiwa kuifanya na kupelekea utekelezaji wa miradi hiyo kuwa wa kubembelezana na wa kuwaomba kuikamilisha, hali inayopelekea malalamiko mengi katika baadhi ya miradi inayotekelezwa na REA.
Waziri Makamba ameweka bayana kuwa, kuanzia sasa hivi, Wizara ya Nishati itabadilisha masharti mapya ya kutoa zabuni za miradi ya REA ya kuwa, kama Mkandarasi ana kazi ya REA ambayo amepewa na yuko nyuma ya ratiba, basi Mkandarasi asahau kupata kazi nyingine ya REA. Pia kama Mkandarasi amefanya kazi ya REA na huko nyuma na ameisumbua sana Wizara na uongozi wa REA na ameimaliza kazi hiyo nje ya wakati, Mkandarasi huyo asihangaike kuomba kazi nyingine ya REA kabisa kwani hatapata.
Waziri Makamba amesisitiza kuwa, ni bora kubaki na wakandarasi watatu au wanne wenye uwezo kuliko kuwa na wakandarasi 50 wasio na uwezo.
Amesema katika kuchagua wakandarasi, ni muhimu kuchagua wakandarasi wenye uwezo wa kufanya kazi na wenye historia ya kufanya kazi hizo na kuwa kuliko kuwa na wakandarsai wasio na uwezo, na wenye kufanya kazi kwa kusua sua, Wizara ya Nishati iko tayari kutafuta mkandarasi mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi hizo kutoka nchi nyingine duniani.
Amesema cha muhimu ni kazi ifanyike na si kuwajengea watu uwezo wa kujifunza namna ya kufikisha umeme vijijini. “Kama hamwezi kufanya hiyo kazi kaeni pembeni”. Alisisitiza Waziri Makamba.
Kufuatia hatua hiyo, Waziri Makamba amesema mkandarasi ambaye kwa sasa ana asilimia 28 tu ya utekelezaji, hatamruhusu mkandarasi huyo kusaini mkataba mpya wa REA.
Aidha, Waziri makamba ameonya kuwa, iwapo kasi ya utekelezaji wa miradi kwa mkandarasi itabakia ile ile wanayokwenda nayo kwa sasa basi hii itakuwa ni fursa ya mwisho kwa mkandarasi huyo kupata kazi za REA na kuwaomba wakandarasi hao wapeleke ujumbe huo kwa Wakandarasi wengine wote wa REA ambao hawajasikia ujumbe huo.
Vile vile, Waziri Makamba amebainisha kuwa, Wizara inaanza program ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. Kwani tayari serikali imefikia asilimia 75 katika kufikisha umeme vijijini na kuwa wakati ikiwa katika hatua ya kumalizia kufikisha umeme vijijini kwa asilimia 25 iliyobakia, tayari Wizara inapeleka Serikalini program kubwa ya fedha kwa ajili ya kupeleka umeme vitongojini.
“Tunapeleka umeme kwenye visiwa, migodini, kwenye viwanda vidogo vidogo, kwenye maeneo ya uzalishaji wa mashambani, viwanda vidogo vya kusindika mazao, migodi na tunazo fedha mahsusi kwa ajili ya kazi hiyo. Umeme tunaoutaka si wa kuwasha taa, bali ni umeme wa kuhamasisha ukuaji wa uchumi, ujasiria mali na uzalishaji mali vijijini. Ndio thamani ya umeme itakapoonekan” alisema Makamba.
Amesema hivi karibuni mikataba imesainiwa kwa ajili ya kazi hiyo. Hivyo kuna kazi nzuri inaendelea ya kuhakikisha kwamba penye shughuli za kiuchumi na huduma muhimu kwa jamii umeme ufike.
Waziri Makamba ameitaka menejimenti ya REA ikakae na kutafakari namna gani wanaweza kufanya mabadiliko katika usimamizi wa kazi za REA na waje na kitu kinaitwa REA 2.0 ambayo inamaanisha REA mpya. Onekaneni. Kuweni na meno. Alisisitiza Waziri Makamba
Pia, amewataka waratibu wa miradi ya REA katika kila mkoa na Wilaya kuweka mfumo wa mawasiliano ya moja kwa moja baina yao na makao Makuu ya Wizara kusimamia utekelezaji.
Naye Naibu Waziri wa Nishati Wakili Stephen Byabato amesema kulikuwa na changamoto mbalimbali kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi ya REA hivyo hatua ya kuwa pamoja na wakandarasi na kuwasimamia kutasaidia katika utekelezaji mzuri wa Miradi ya REA.
Amewataka wakandarasi hao kukamilisha miradi kwa wakati na kuwa jukumu la usimamizi wa utekelezaji wa Mradi huo wa Peri Urban III litakuwa ni jukumu lake la msingi ikiwa ni katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwafikishia wananchi wote umeme.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kwa miaka mingi kuna maeneo ya pembezoni mwa miji ambayo yana maendeleo mazuri, nyumba nzuri zimejengwa na pana wateja wazuri wenye uwezo wa kutumia umeme, lakini kwa sababu mbalimbali, TANESCO imekwenda mpaka kiwango fulani na bado kuna maeneo haijayafikia.
Mramba ameeleza kuwa hii si kwa sababu TANESCO haioni haja ya kupeleka umeme katika maeneo hayo, bali ni kutokana na ukweli kuwa, majukumu ya TANESCO ni mengi na yanaenda kwa hatua.
“Mradi huu, unasaidia kuwafikishia umeme wateja wale ambao kwa kiasi kikubwa wapo tayari kupokea umeme lakini tu miundo mbinu ya umeme haijafika maeneo hayo. Mradi wa Peri Urban ambao umeenda hatua kwa hatua, naamini ni jibu la kuweza kufikisha umeme katika maeneo hayo.” Alisema Mha. Mramba.
Katibu Mkuu Mramba amesema, nia ya uongozi wa Wizara ya Nishati ni kuona kuwa kazi hii inafanyika kwa kasi kubwa kwa sababu miundombinu ipo na kazi ya Wakandarasi ni kufanya muendelezo (extension) kwa ajili ya kuwafikia wateja husika hivyo ni matarajio ya Wizara ya Nishati kuwa, kazi hiyo itafanyika kwa haraka, lakini pia kwa ubora na kwa umakini. Ili wateja hao wapate umeme katika viwango vinavyokubalika.
Katibu Mkuu Mramba amewataka wakandarasi hao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, kwa ubora na kwa kukidhi matarajio na malengo ya miradi ilipokuwa inaanzishwa.
Mradi wa Peri Urban III ni jibu katika kufikisha umeme katika maeneo ambayo TANESCO imepeleka umeme kwa kiwango fulani lakini kuna maeneo ambayo haijayafikia si kwa sababu TANESCO haitaki kufikisha umeme katika maeneo hayo bali ni kutokana na ukweli kuwa majukumu ya TANESCO ni mengi na yanakwenda kwa hatua
Awali, akizungumza na wakandarasi hao, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mha. Hassan Saidy, aliwataka wakandarasi kutumia hekima na ushirikishwaji wa wananchi husika pamoja na viongozi wao ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima wakati wa utekelezaji wa mradi.
Mha. Saidy, amewataka wakandarasi hao kushusha vifaa katika maeneo husika ya mradi ili kuepuka usumbufu wa kuwa na mvutano na wananchi unaotokana na wakandarsai kushusha vifaa kwenye eneo lisilo la mradi na baadae kutaka kuvihamisha kwenda kwenye eneo la mradi.
Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wengine waliosaini mikataba ya Peri Urban III na REA, Mrisho Masoud wa Kampuni ya OK Electrical and Electonics Services LTD, amemwakikishia Waziri Makamba kuwa watatekeleza miradi hiyo kwa ufanisi na pia wametambua kuwa Waziri Makamba hana mzaha katika kazi.
Mradi wa Peri Urban awamu ya tatu utapeleka umeme kwenye maeneo 416 katika mikoa 8 ya Mtwara, Singida, Mbeya, Geita, Tabora , Kagera, Kigoma na Tanga ukihusisha ujenzi wa njia za msongo wa kati wa umeme zenye urefu wa 447km, njia za msongo mdogo wa umeme za urefu wa 1020km, kufunga transformer 417 pamoja na kuunganisha wateja wa awali 22,105 kwa gharama ya shilingi Bilioni 76.9.