Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Steven Lukanga akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wachakataji wa mazao ya uvuvi Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Na Devotha Songorwa, KIGOMA.
Wachakataji wa mazao ya uvuvi nchini wametakiwa kutumia fursa ya teknolojia katika shughuli zao ili kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi na kukabiliana na upotevu wa mazao hayo katika Ziwa Tanganyika.
Hayo yameelezwa na Afisa Mtaalam Mnyororo wa Thamani wa Uvuvi na Ufugaji Viumbe Maji Hashim Muumin wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wachakataji, wavuvi na wafanyabiashara yaliyoandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kupitia miradi yake ya FISH4ACP na Flexible Multi-partner Mechanism (FMM) mafunzo ambayo yamefanyika mkoani Kigoma.
Afisa huyo amesema mradi wa FISH4ACP unatekelezwa katika nchi 12 za Africa, Caribbean na Pacific ambapo nchini Tanzania unafanyika katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma ukilenga kukabiliana na changamoto za upotevu wa mazao ya samaki kabla na baada ya shughuli za uvuvi, wakati wa uchakataji wa samaki na wakati wa kusafirishwa kwenda kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Mafunzo haya yamefanyika kwa njia ya filamu zilizonakiliwa kutoka Kenya, Uganda na Ghana lengo ni kuwawezesha wachakataji kujifunza njia bora za kuchakata mazao yao kama tulivyoona kwa wenzetu wanatumia majiko banifu, chanja rafiki na salama za kuanikia dagaa,”Amesema Afisa huyo.
Pia ameongeza kuwa kupitia miradi hiyo wanatarajia kujenga miundo mbinu ya kuchakatia dagaa na samaki itakayoendana na mabadiliko ya tabia Nchi ambapo kwa sasa hatua zilizochukuliwa ni ufuatiliaji wa maeneo sahihi ya kuchakatia.
“Kama mradi tutatengeneza majiko ya kubanikia samaki tupate bidhaa nzuri kutoka Ziwa Tanganyika na tutaendelea na ufuatiliaji kuona kama mafunzo haya yanatafanya kazi kama tulivyokusudia na yatasaidia changamoto iliyopo sasa ya mabadiliko ya tabianchi ,”Ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala la Udhibiti Ubora wa Mazao ya Uvuvi na Masoko, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Bw. Steven Lukanga amebainsiha kuwa sekta ya uvuvi inachangia karibu asilimia 1.8 ya pato la Taifa wakati ulaji ukichangia asilimi 30 ya virutubishi vitokanavyo na wanyama.
“Ulaji wetu unaonekana tunakula wastani wa kilo 8. 5 badala ya kilo 20.5 kwa mwaka hivyo mafunzo haya yamekuja wakati muafaka yatasaidia kuboresha shughuli zetu tunazofanya hasa unapovua samaki wako au dagaa uhakikishe unawahifadhi sehemu salama na hata ukaushaji wetu uwe wenye manufaa kimasoko,”Amefafanua.
Naye Afisa Uvuvi anayesimamia Wilaya ya Uvinza Venance Msongambele amesema elimu hiyo itawasaidia wadau wa uvuvi na wachakataji kuepuka kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake watakausha samaki kwa kutumia mkaa hatua inayoongeza thamani ya mazao hayo na kuvutia wateja.
“Kuna maboresho ambayo yakifanyika yatatusaidia sana kama kupata barafu kuhifadhi samaki na dagaa, majiko ya mkaa kwa sababu kuni siyo salama kwa afya kutokana na moshi na kupitia mafunzo haya tumejifunza kufanya uchakataji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira,”Ameeleza Afisa huyo.
Akitoa shukrani zake Mchakataji kutoka Mwalo wa Katonga mkoani Kigoma Selestina Silvester ameipongeza FAO kwa kuandaa semina hiyo kwani itawasaidia katika uhifadhi wa rasilimali za Ziwa Tanganyika kwa manufaa yao na Nchi kwa ujumla.
“Tunaishukuru sana FAO kwa kutoa na elimu hii inatusogeza kutoka hapa tulipo hadi sehemu nyingine kwa sasa uchakataji tunafanya kienyeji sasa unakuta samaki au dagaa wanaharibika haraka kabla ya kufika sokoni na wanapungua ubora,”Amesema Selestina.
Aidha Mwenyekiti wa Vyama vya Wavuvi Mkoa wa Kigoma Bwa. Francis John amewahimiza wadau hao kutumia ujio wa mradi huo kama fursa muhimu kwao kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuendana na hali ya soko la sasa.
Baadhi ya wadau wa sekta ya uvuvi wakiafuatilia mafunzo hayo kutoka kwa wawezeshaji(hawapo pichani).