Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GARI LA WAGONJWA 'AMBULANCE' LAUA MUUGUZI NA MAMA MJAMZITO KWENYE KONA SPIDI KALI KUELEKEA HOSPITALI

Mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 21, na mtoto wake aliyekuwa tumboni walifariki dunia wakati gari la wagonjwa lililokuwa likimkimbiza hospitalini kupoteza mwelekeo na kuanguka.


Ripoti zinaeleza kuwa muuguzi wa kiume aliyekuwa ameandamana na mwanamke huyo pia alifariki dunia katika ajali hiyo mbaya iliyotokea kwenye kona ya barabara ya Hospitali ya Mukobeko nchini Zambia. 

Zambia Daily Mail inaripoti kuwa ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa kumi na mbili jioni, dereva ndiye analaumiwa kwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi zaidi wakielekea hospitalini.


Mama huyo mjamzito Agatha Chanda na muuguzi Simon Lukama walikuwa safarini kuelekea Hospitali Kuu ya Kabwe ambako alipewa rufaa kutoka Kliniki ya Katondo walipopata ajali.


“Kutokana na mwendo wa kasi, gari la wagonjwa lililokuwa likiendeshwa na Charles Makasa (40), lilipoteza mwelekeo barabarani na kugonga mti,” ilisoma sehemu ya ripoti hiyo.

 Aliyekuwemo pia ndani ya gari hilo ni mamaake Chanda, Ellen mwenye umri wa miaka 41, ambaye alinusurika kifo lakini alipata majeraha pamoja na dereva wa gari hilo la wagonjwa. 

Maoni kutoka kwa wananchi yaligawanyika kuhusu iwapo dereva ndiye anapaswa kulaumiwa kwa kuendesha gari kwa kasi katika juhudi za kuokoa maisha.

Kufuatia ajali hiyo mbaya, wananchi walimlaumu dereva wa gari hilo la wagonjwa kwa mwendo wa kasi.

Wengine, hata hivyo, walihoji kwamba dereva huyo hakuwa na makosa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi kwani alikuwa akijaribu kuokoa maisha ya mama na mtoto.

 Warren Chisanga: "Kabla ya kumlaumu dereva, wafanye uchunguzi wa kina wa gari ambalo limetajwa kuwa ni gari la wagonjwa na kama linafaa kuwa barabarani. Ikiwa ni dharura dereva hawezi kutembea polepole."

Cyn Chuma Sibeso: "Tunaelewa magari ya kubebea wagonjwa hayatakiwi kutembea taratibu lakini niamini madereva hawa wanatia chumvi. Nimebebwa na kadhaa, hawa jamaa huhisi wanamiliki barabara."

 Patricia Chikwete: "Kuokoa maisha inakuwa haina maana pale mtu anapozembea kuendesha gari. Madereva hawa wanaweza kuongeza kasi, jambo ambalo si salama." 

Elita T Mwanza: "Alikuwa anaendesha kwa kasi ili wawahi hospitali kwa wakati kwa sababu kuzaa mtoto ni suala la maisha na kifo."

Via - Tuko news

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com