The Academy Universal Global Peace yenye Chuo Kikuu Cha The American University Global Peace chenye matawi nchi 120 duniani ikiwemo Tanzania kinachoongozwa na Profesa Madhu Krishan kimemtunuku Tuzo ya Heshima Kamanda wa Polisi Ilala Dar es salaam ACP Debora Magiligimba.
Kufuatia Tuzo hiyo ya Heshima Kamanda wa Polisi Ilala ACP Debora Magiligimba, sasa ni Dr. ACP Debora Magiligimba.
Chuo hicho katika mwendelezo wa kuwachunguza watu waliogusa kazi za kijamii duniani kimemgundua Mfanyakazi wa Jeshi la Polisi Tanzania ACP Debora Magiligimba kuwa ni mwanamke Shujaa aliyefanya kazi nyingi za jamii.
Chuo hicho kimemfuatilia ACP Debora Magiligimba kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Youtube na njia zingine na kugundua kuwa amejikita sana kwenye shughuli za jamii hususani masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambapo amekuwa akijitoa katika kuelimisha jamii kujiepusha vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukemea vitendo vya kikatili kupitia makongamano, mikutano ya wananchi, kutoa elimu kwenye nyumba za ibada,kutoa elimu kwa wake za askari na askari wenyewe, kutatua migogoro ya ndoa, kutoa elimu kwa njia ya Tv na Redio.
"Katika kumfuatilia tumebaini kuwa mikoa yote aliyowahi kufanya kazi vituo tofauti pamoja na majukumu mbalimbali amefanya kazi nyingi za kugusa jamii. Kwa kazi nyingi alizofanya katika jamii tumeona ni Mwanamke kiongozi wa tofauti anayestahili kutunukiwa Tuzo ya Heshima",amesema Profesa Madhu Krishan.