Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye (kushoto) akimjulia hali mmoja wa wakazi wa Kishapu waliojeruhiwa kwa kushambuliwa na fisi ambapo sasa wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu. UWT Mkoa wa Shinyanga wametembelea hospitali hiyo na kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM
Na Halima Khoya - Shinyanga
Jumuiya ya Umoja wa Umoja wa Wanawake Mkoa wa Shinyanga imeadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu kwa kupanda miti, kutembelea na kuwapa zawadi wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu.
UWT wakiongozwa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye
pia wamewajulia hali watu wanne wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Mwalata Mkoani Shinyanga waliojeruhiwa kwa kushambuliwa na fisi sehemu mbalimbali za miili yao.
Tukio hilo la kushambuliwa na fisi limetokea Januari 30,2023 majira ya saa 7 usiku katika kijiji cha Mwalata Kata ya Ndololeji Halmashauri ya wilaya Kishapu Mkoani humo.
Akieleza juu ya tukio hilo, mama mzazi wa majeruhi wawili (Jishansa Kija mwenye miaka 18 na Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la 5), Bi. Mbuko Jishanga amesema kuwa majira ya saa saba usiku alisikia kelele nje ya nyumba yake ndipo alipotoka na kumkuta mwanae Jishansa akiwa amejeruhiwa usoni pamoja na Emmanuel akiwa amejeruhiwa kichwani.
Jishanga amesema kuwa mara baada ya kukuta hali hiyo alimuagiza panga Mkwilima wake Malambi Mayara,ambaye baada ya kumjeruhi fisi huyo kichwani alimrukia kijana huyo ambapo aling'ata shingoni na kufanikiwa kumuua akiwa ameng'ang'ania kwenye mwili wa Mkwilima huyo.
"Majira ya saa 7 usiku nilisikia kelele nje,nilipotoka niliwakuta wanangu wakiwa wamejeruhiwa na fisi ikabidi nimuagize mtoto panga nikawa namvizia fisi huyo atoke nje na alipotoka tu alikutana na panga la kichwa akaanguka,alipoamka tena nikamkata mara ya pili huku nikiwa napiga kelele,watu walijaa wakanisaidia kumuua vizuri pamoja na kuwaleta watoto hospitali", amesema Jishanga.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya Kishapu,Dr Mohamed Mkumbwa, amesema majira ya saa 10 alfajiri tarehe 30,2023 amepokea wanaume 4 wakiwa wamejeruhiwa maeneo mbalimbali ya miili yao ambao walipatiwa huduma za kimatibabu na kufikia sasa hivi hali zao ni nzuri.
Akizungumza baada ya kutembelea Hospitali ya Jakaya Mrisho Kikwete ya Wilaya ya Kishapu, Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Helen Bugoye ameeleza kusikitishwa na tukio hilo huku akiwataka wakazi wa Kishapu kushirikiana na Mamlaka zinazohusika kudhibiti wanyama wakali kuwawinda wanyama hao.
"Wanawake tunaweza,kwani mzazi mwenzetu amewapambania watoto wake ambao walikuwa wamevamiwa na fisi, inatakiwa mamlaka ya maliasili wafike kwenye kijiji hiki ili kuwawinda wanyama hatarishi", amesema Bugoye.
Social Plugin