VIJANA WANNE WA FAMILIA MOJA WANUSURIKA KUFA KWA KUSHAMBULIWA NA FISI KISHAPU,... MAMA MWENYE PANGA ATISHA

Mnyama Fisi

Na Sumai Salum - Kishapu
Wanaume wanne wa familia moja katika kijiji cha Mwalata Kata ya Shagihilu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kushambuliwa na mnyama Fisi wakiwa wanalinda mbuzi na ng'ombe nyumbani kwao. 


Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Kishapu Bw. Mohamed Mkumbwa amesema waliwapokea majeruhi majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia leo Jumatatu Januari 30,2023 wakiwa na hali mbaya  na baada ya kuwapa huduma sasa wanaendelea vizuri.


"Ni kweli tumewapokea majeruhi wanne alfajiri ya leo wakiwa na hali si nzuri ,kuna aliyejeruhiwa kwa kung'atwa chini ya pua mwingine kichwani mwingine mapajani na mwingine sehemu ya kichwani kuelekea shingoni na sasa tunamshukuru Mungu wanaendelea vizuri", ameeleza Dkt. Mkumbwa.


Waliojeruhiwa ni Jishanga Izengo (18) aliyejeruhiwa sehemu ya chini pua, Kanizio Joseph mwanafunzi anayesoma darasa la 4 shule ya msingi Mwalata aliyejeruhiwa maeneo ya mapajani, Lazaro Emmanuel anayesoma darasa la 5 shule ya msingi Mwalata aliyejeruhiwa maeneo ya kichwani na mikononi pamoja na Malambi Mayala ambaye amejeruhiwa sehemu ya kichwani kuelekea shingoni na wote wameshonwa majeraha yao.


Akisimulia kuhusu tukio hilo, mama mzazi wa watoto hao, bi.Mbuke Jishanga Izengo amesema kuwa mnamo majira ya saa 7 usiku wa kuamkia leo tarehe 30 alimsikia kijana wake Jishanga akipiga kelele hivyo alivyotoka nje akakuta wameshambuliwa na fisi ambaye baadaye alichukua panga na kuanza kupambana naye huku akipiga kelele majirani zake wakaja kumsaidia.


"Yaani huyu fisi angeniulia watoto wangu sisi kwetu huwa tuna desturi ya watoto wa kiume kulinda mifugo ikiwemo mbuzi na ng'ombe hivyo wakati wamelala ndipo akaja fisi kuanza kuwashambulia kwa kweli nikaona nichukue panga nianze kupambana nae nikamkata eneo la kichwa akaenda kujibamiza ukutani mwa nyumba akapanga mipango ya kunirudia na mimi nikaweka panga vizuri akaja, nikamkata tena akalala na watu wakaja tunamalizia. Nashukuru Mungu amewasaidia na sasa wanaendelea vizuri", amesema Mbuke.

Kijana mkubwa wa familia hiyo anayejulikana kwa jina la Joseph Shija amesema kuwa fisi huyo wanamhusisha na imani za kishirikina.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post